MADRID, Hispania
LICHA ya Barcelona kung’olewa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kinda wake wa safu ya ushambuliaji, Lamine Yamal, ameitumia mechi yao dhidi ya Atletico Madrid kuweka rekodi mbili.
Barcelona walikwenda ugenini wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 2-0 katika robo fainali ya kwanza. Walishinda mabao 2-1 jana Aprili 14, 2026 lakini wametolewa kwa matokeo ya jumla (3-2).
Wakiwa ugenini jana, Yamal aliitanguliza Barcelona katika dakika ya nne tu ya mchezo, akitumia ‘asisti’ ya Ferran Torres.
Hivyo, Mhispania huyo amekuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi (miaka 18 na siku 275) kufikisha mabao 20 kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa.
Wakati huo huo, Yamal amekuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kupachika mabao 10 ndani ya msimu mmoja wa mashindano hayo ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA).
Awali, rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Erling Haaland aliyefanya hivyo akiwa na miaka 19 na siku 212, wakati huo akiitumikia Red Bull Salzburg ya Austria.






