
KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Mary Kanumba, amewataka wachimbaji wa madini katika eneo la Londoni kuwa chachu ya maendeleo kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali katika ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza katika kikao cha kujadili mbinu bora za kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya madini, Mary amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wachimbaji na serikali za vijiji ili kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Amebainisha kuwa sekta ya madini ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa halmashauri, huku akiwataka watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo katika kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji, ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi.
Kwa upande wao, wachimbaji wamewasilisha mapendekezo mbalimbali likiwemo kuboreshwa kwa miundombinu ya uchimbaji ili kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Mwenyekiti wao, Abdallah Mfaume, ameiomba Serikali kuongeza ziara za mara kwa mara katika maeneo ya uchimbaji ili kutambua changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.






