PANDE zote mbili zinatupiana lawama, kila moja ikiitaja nyingine kukwamisha upatikanaji wa suluhu katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika mjini Islamabad, Pakistan.
Wawakilishi wa Marekani na Israel walikutana Pakistan kwa mazungumzo ya kutafuta suluhu ya vita vilivyodumu kwa wiki sita (tangu Februari 28, 2026).
Mkutano wa Islamabad ni wa kwanza kwa viongozi wa Marekani na Iran kufanya mazungumzo ya ana kwa ana baada ya miaka zaidi ya 10 kupita.
Licha ya mazungumzo hayo kuchukua saa 21, hakuna makubaliano yaliyofikiwa, hivyo kuibua hofu kwamba huenda vita kati ya pande hizo vikaendelea Mashariki ya Kati.
Maofisa wa Marekani wameeleza kuwa mazungumzo yameshindwa kufikia pazuri kwa sababu Iran imegoma kuachana na programu ya nyuklia.
“Tunataka kuona dhamira yao ya kuachana na silaha za nyuklia, na hawatotafuta zana za kuwawezesha kupata silaha za nyuklia,” amesema Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance.
Kwa upande wao, viongozi wa Iran hawajaeleza sababu lakini wamedai kuwa Washington ndiyo chanzo cha kukosekana kwa makubaliano.
Kiongozi wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo, ambaye pia ni Spika wa Bunge la nchi hiyo, Mohammad Bagher Qalibaf, amesema: “Ni wakati wa Marekani kuamua kama inaweza kutumiani.
Hata hivyo, Shirika la Habari la Iran, Tasnim, limeeleza kuwa matakwa makubwa ya Marekani kwa Iran ndiyo sababu ya kukwamisha kupatikana kwa mwafaka katika mazungumzo hayo.
Chanzo kingine cha habari kimeeleza kuwa mbali ya nyuklia, pia Marekani iliitaka Iran kuachia udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Mchambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati, Fatemeh Aman, amesema takwa la Iran kutaka iondoshewe vikwazo ilivyowekewa na Marekani ni kizingiti kingine kilichokwamisha kupatikana kwa suluhu.
Lakini, kwa mujibu wa mchambuzi mwingine, Farwa Aamer, masuala ya nyuklia na Mlango-Bahari wa Hormuz yamechangia mazungumzo kuwa magumu.
“Pande zote mbili zilikutana zikiwa na mtazamo na msimamo tofauti juu ya nyuklia na Mango-Bahari,” amesema
Kwa upande wake, Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mazingira ya pande mbili kutokuaminiana yamesababisha kukosekana kwa suluhu katika mazungumzo ya Islamabad.
Wakati huo huo, baadhi ya wachambuzi wanapata hisia kuwa kukosekana kwa suluhu kumeyaacha njiapanda makubaliano ya awali ya kusitisha vita kwa wiki mbili.
Kwamba huenda vita vikarudi. “Ni kweli wako kwenye makubaliano ya kusitisha (kwa wiki mbili) lakini hayako imara,” anasema Fatemeh.
“Makubaliano yao hayana msingi wa kisiasa (kama ambayo yangefikiwa Islabamad. Kila upande una uwezo wa kuamua (kuendelea na vita ama la).”






