Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, limefanikiwa kuwaokoa watu nane waliokuwa wamezingirwa na maji kufuatia mvua kubwa zilizosababisha mafuriko.
Tukio hilo limetokea leo Aprili 11, 2026 majira ya saa 07:45 asubuhi katika kijiji cha Koboko Kusini, Kata ya Nasai wilayani Siha, baada ya maji kuingia kwenye makazi ya wananchi na kuwazuia kutoka nje.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Siha, askari walifika eneo la tukio kwa wakati na kuanza operesheni ya uokoaji, ambapo walifanikiwa kuwaokoa watu wote waliokuwa wamekwama ndani ya nyumba zilizozingirwa na maji.
Waliookolewa ni watu wazima wawili pamoja na watoto sita, wote wakiwa wa jinsia ya kike. Aidha, watu wengine wanne waliripotiwa kuathirika na tukio hilo.






