LUSAKA, Zambia
WIZARA ya Afya ya Zambia imekuwa ikinufaika na misaada ya afya kutoka Marekani lakini wakosoaji wanasema kuna siri nzito inayoendelea nyuma ya pazia.
Marekani imekuwa ikiipatia Zambia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu (TB) na malaria.
Watu zaidi ya milioni moja nchini humo wana maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Marekani imekuwa ikitoa misaada, ikiwamo kuchangia bajeti ya matibabu ya ugonjwa huo.
Kwa msaada wa Marekani, Zambia imepata matokeo chanya katika kukabiliana na ugonjwa huo, ambapo maambukizi mapya yamepungua kutoka 63,000 hadi 30,000 kati ya mwaka 2010 na 2025.
Hata hivyo, kwa jicho la wakosoaji, Marekani imekuwa ikiitumia misaada hiyo kujichotea madini yanayopatikana katika Taifa hilo la Kusini mwa Afrika.
Takwimu zinaonesha, Zambia inashika nafasi ya pili kwa kiwango kikubwa cha uzalishaji wa madini ya shaba barani Afrika.
Machi 2026, Gazeti la New York Times lilifichua kile kilichoelezwa kuwa ni ujumbe wa Katibu Mkuu wa Ikulu ya Marekani, Marco Rubio, kwa Serikali ya Zambia.
Katika ujumbe huo, Rubio aliishinikiza Zambia, kama ilivyofanya kwa mataifa mengine 23 yanayopokea misaada, kukubaliana na matakwa ya Marekani.
Pamoja na masharti mengine, Zambia ilitakiwa kuiruhusu Marekani kuyafikia madini muhimu ya shaba, nickel na cobalt.
Taasisi ya wanaharakati wa masuala ya afya ya HealthGAP ya Zambia inasema nchi yao haipaswi kuingia kwenye makubaliano ya aina hiyo, yanayoruhusu rasilimali zao kuibiwa kwa kivuli cha misaada.
Tangu Marekani ilipojitoa katika Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), imekuwa ikiingia makubaliano na mataifa ya Afrika yanayohitaji msaada wake katika masuala ya afya.
Misaada hiyo, kwa mujibu wa wakosoaji, imekuwa ikiambatana na gharama ya mataifa hayo kuiachia Marekani baadhi ya rasilimali muhimu, yakiwamo madini.
Miongoni mwa nchi 23 zilizosaini makubaliano hayo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wakati Kenya na Zimbabwe zimetajwa kugomea.






