SERIKALI ya Marekani imekataa rasmi mapendekezo ya hoja 10 yaliyowasilishwa na Iran kuhusu kusitisha mapigano, ikisema masharti hayo hayaendani na msimamo wake wa kiusalama.
Mpango wa Iran ulihusisha mambo kadhaa ikiwemo kuendelea na shughuli za nyuklia na kuondolewa kwa majeshi ya Marekani Mashariki ya Kati, mambo ambayo Washington imeyapinga vikali.
Marekani imesisitiza sera yake ya kutokubali urutubishaji wa nyuklia, huku ikiweka wazi kuwa haitapunguza uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.
Tofauti pia zimejitokeza kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambapo Iran inataka ushawishi mkubwa zaidi, lakini Marekani inataka njia hiyo ibaki wazi kwa biashara ya kimataifa.
Pamoja na mvutano huo, juhudi za mazungumzo bado zinaendelea, huku pande hizo zikitarajiwa kukutana ana kwa ana kujadili mustakabali wa amani katika ukanda wa Mashariki ya Kati.






