![]() |
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi, Ramadhani Kingai |
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Ravji Construction Limited yenye makao makuu yake mkoani Kilimanjaro imeibua madai mazito ya utapeli, kughushi nyaraka na sahihi dhidi ya Kampuni ya Mohamed Enterprise Tanzania Limited (MeTL) yenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam.
Katika madai yake hayo, Ravji Construction Ltd inaituhumu MeTL kuitapeli Dola za Marekani 600,000 kwa kuiuzia kiwanja ambacho si mali yake na kughushi nyaraka na sahihi za makubaliano ya mauziano hayo.
Govind Varsani Ravji, ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa, mapema mwaka 2011 akiiwakilisha Kampuni ya Ravji Construction Ltd alianza kufanya mazungumzo na afisa mmoja wa ngazi za juu wa MeTL aliyemtaja kwa jina ka Murtaza Alihussein Dewji kuhusu kununua kiwanja namba 105, kilichopo Mbezi, eneo la viwanda kwa gharama ya Dola za Marekani 700,000, ambacho MeTL ilieleza kuwa ni mali yake.
Ravji anasema mazungumzo hayo yalizaa matunda mwishoni mwa mwaka 2011 ambapo kampuni yake ililipa fedha ya mwanzo Dola za Marekani 600,000 kwa MeTL lakini katika hatua ya kushangaza, MeTL baada ya kupokea malipo hayo ilipandisha dau na kutaka ilipwe Dola za Marekani 800,000.
“Malipo yote tulilipa kwa Kampuni ya METL na aliyeingia makubaliano ya kutuuzia ardhi hiyo ni Murtaza. Sasa walipopandisha bei hatukuwa na kipingamizi lakini tuliwaomba watupe kwanza hati ya kiwanja na hapo ndipo sokomoko lilipoanzia.
“Nilimwambia Murtaza watupatie hati ili na sisi tuwamalizie Dola za Marekani 200,000 zilizobakia lakini alisema hati imepotea. Baadaye kidogo tukaambiwa kuwa bei tuliyokubaliana siyo Dola za Marekani 700,000 bali ni Dola za Marekani Milioni 1.2 hapo tukashtuka lakini wao wakawa na nyaraka hizo za makubaliano ya Dola za Marekani Milioni 1.2, tukavutana mpaka mwaka 2014 bila kuafikiana tukajua tumetapeliwa na hawa jamaa, tukakimbilia polisi,” anasema Ravji.
Anaeleza zaidi kuwa baada ya mvutano wa muda mrefu walifungua malalamiko kituo cha polisi Kawe, mwaka 2014 na uchunguzi wa hati hizo za MeTL za makubaliano ya mauziano ya Dola za Marekani Milioni 1.2 ulifanywa na maofisa wa kitengo cha Forensic.
Huku akionyesha nyaraka, anasema; “Matokeo ya uchunguzi huo wa kitaalamu uliofanywa na polisi ulibainisha kuwa Murtaza alighushi nyaraka na sahihi zinazoonyesha kuwa tulikubaliana kuuziana kwa Dola za Marekani Milioni 1.2, na uchunguzi tuliofanya sisi baada ya kubaini nia ovu ya MeTL ulionyesha kuwa hiyo ardhi ambayo MeTL walitaka kutuuzia haikuwa mali yao wala haikuwa mali ya Murtaza Alihussein Dewji.
“Uchunguzi wa nyaraka ulibainisha kuwa ardhi ile ni mali ya Aliraza kasamali Rajani. Sahihi zilizo kwenye hizo nyaraka zinaonyesha namba ya simu ya nje ya nchi na hata sahihi zake mbili zilizopo zinatofautiana.”
Anasema tangu uchunguzi huo ulipokamilika mwaka 2014 hadi sasa ukiwa umebainisha MeTL kughushi nyaraka na sahihi, hakuna kesi iliyofunguliwa mahakamani hivyo baada ya kusubiri kwa miaka mingi ili kuchukuliwa hatua zitakazowarudishia haki yao, sasa wameamua kuomba huruma ya Rais Dk. John Magufuli aingilie kati sakata hilo.
![]() |
Gulam Dewji |
Mmiliki wa Kampuni ya MeTL, Gulam Dewji bado hajapatikana kuzungumzia madai hayo kwa sababu amekuwa hafiki ofisini kwake na alipowasiliana na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni alieleza kuwa yupo nyumbani anaumwa hivyo hawezi kulizungumzia jambo hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi, Ramadhani Kingai alipoulizwa alisema hana taarifa za kuwepo kwa kesi hiyo lakini amemuagiza Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Kinondoni kufuatilia na kumpatia taarifa ni wapi faili la kesi hiyo lilipokwama.
“Sina details za kesi hiyo, niseme siijui kabisa. Lakini nimeyaona maswali yako na mimi nimemuagiza RCO afuatilie na anipe taarifa ni wapi faili la kesi hiyo lilipokwama. Kesi yenyewe hiyo naona ni ya muda mrefu, hii ilitokea mimi nikiwa sipo hapa. Lakini Alhamis au Ijumaa nitakuwa na taarifa kamili, nitafute mwishoni mwa wiki nitakupa taarifa kamili kuhusu kesi hiyo,” alisema Kamanda Kingai.