TERESIA MHAGAMA
DODOMA
SERIKALI imesema, gharama za kununua umeme hazijapanda.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewea hivi karibuni jijini Dodoma na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi alipokuwa akizungumza na watumishi wa wizara hiyo, taasisi zilizo chini ya wizara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Alisema gharama za vifaa vya umeme ambazo ni nguzo, waya na mita ndivyo vilivyopanda bei lakini serikali haijapandisha bei ya umeme kwa muda wa miaka 10 sasa.
“Kiwango cha uunganishaji wa umeme nchini kimefikia asilimia 52 na serikali imeweka lengo la kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2030 linalotekelezwa kupitia mpango wa nishati uliosainiwa januari 2025 wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika,” alisema.
Kuhusu suala la mita janja, waziri huyo alisema kazi ya uunganishaji wa mita hizo inaendelea nchi nzima na zitamwezesha mwananchi kupata umeme mara moja baada ya kununua token bila kutumia kifaa cha ziada cha kuingiza namba (CIU).
Waziri Ndejembi alizungumzia pia upatikanaji wa umeme wa gridi mkoani Rukwa kwa kueleza kuwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 unaendelea kutekelezwa kupitia mkandarasi anayejulikana kwa jina la TBEA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, alilipongeza Shirika la Ugavi wa Umeme
(TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusambaza umeme nchini.
Alisema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
