TERESIA MHAGAMA,
DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza kuridhishwa kwake na kazi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa muda wa siku 100 alizokaa ofisini tangu alipoanza awamu ya pili ya uongozi wake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dodoma alipokuwa akiongoza kikao cha kwanza cha kamati yake, Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.
Mgalu alisema siku 100 za rais ofisini, umeme umeanza kusambazwa katika vitongoji 9,009 jambo linaloonyesha mwelekeo chanya wa utendaji kazi katika kipindi cha pili cha serikali ya awamu ya sita.
“Niwapongeze sana Wizara ya Nishati na taasisi zilizo chini ya wizara kwa kazi nzuri mnayofanya. Mmepata mafanikio makubwa ndani ya siku 100 ambazo rais wetu amekaa ofisini kwa kipindi cha pili.
“Ndani ya muda huu wa siku 100 tumeona uzinduzi wa kituo cha umeme cha Mtera ambacho kitaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Dodoma na Iringa pamoja na uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 nchini,” alisema Mgalu.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi alisema wizara itaendelea kuchangia ipasavyo ukuaji wa Sekta ya Nishati kitaifa na kimataifa.
Alisema serikali inakusudia kuendeleza matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati ili mpango wa kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030 ufanikiwe.
“Wizara pia itahakikisha matumizi ya umeme kwa wananchi hadi kufikia wastani wa
kilowati (KWh) 3,000 kwa kila mtu ifikapo mwaka 2050 yanafanikiwa,” alisema.
Kuhusu nishati safi ya kupikia, Ndejembi alisema wizara
inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuongeza vituo vya upatikanaji wa nishatihiyo pamoja na kubuni na kuendeleza teknolojia rafiki kwa mazingira.
Kikao hicho kilikuwa mahususi kwa ajili ya kuijengea kamati uelewa kuhusu muundo na
majukumu ya Wizara ya Nishati, sera na sheria mbalimbali zinazosimamiwa na wizara hiyo katika kuendeleza Sekta ya Nishati.
