RIPOTA MAALUMU
VITONGOJI 159 katika Mkoa wa Lindi vinatarajiwa kupatiwa umeme mwaka huu.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Meneja Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Deogratius Nagu alipokuwa akimtambulisha mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kazi hiyo.
Hafla ya kumtambulisha mzabuni huyo ambaye ni Kampuni ya Jaitech ilifanyika Januari 27, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Mhandisi Nagu alisema serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa huo kwa gharama ya Shilingi bilioni 25.8 ambao utahusisha vitongoji 159 vyenye kaya 5,116.

“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha Shilingi 25,826,594,700.00 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 159 mkoani hapa na leo hii tumefika hapa kumtambulisha mkandarasi na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza.
“REA inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vilivyobaki, hivi tunavyozungumza wakandarasi wanaendelea na kazi na hadi sasa katika vitongoji hivyo vilivyobaki vitongoji 378 vipo kwenye mpango wa kufikishiwa umeme,” alisema Mhandisi Nagu.
Alisema, dhamira ya serikali ni kuhakikisha mwaka 2030 vitongoji vyote nchini viwe vimefikishiwa nishati ya umeme na kwamba REA ikiwa na dhamana hiyo itahakikisha miradiya kimkakati inakamilika.
Aidha Mhandisi Nagu alitoa wito kwa wananchi watakaopitiwa na mradi kutoa ushirikiano ili kumuwezesha mkandarasi kutekeleza kazi ndani ya muda na kwa ubora unaotakiwa.
Pia aliiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushirikiana na REA kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi ya kutokuwepo kwa fidia kwa wale ambao maeneo yao yatapitiwa na mradi na watambue kuwa umeme ni fursa ya kiuchumi na kijamii.
“Tunaomba ushirikiano kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kurahisisha utekelezaji wa mradi ikiwemo kuruhusu mradi kukatiza katika baadhi ya maeneo ya misitu sambamba na kuwa na miundombinu wezeshi kuruhusu kusafirisha vifaa vya mradi maeneo mbalimbali atakapokuwa mkandarasi,” alisema Mhandisi Nagu.
