MAKALA MAALUMU
USHINDANI wa sasa wa Bandari za Tanzania kikanda na kimataifa umeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
Bandari za Tanzania sasa zinatoa ushindani mkubwa dhidi ya bandari za kikanda na kimataifa kwenye ongezeko la shehena zinazohudumiwa hususan katika Bandari ya Dar es Salaam.
Katika kipindi cha miaka minne, miundombinu ya Bandari za Tanzania imeboreshwa, mapato yameongezeka na matumizi ya TEHEMA yameanzishwa. Hayo yameiwezesha Tanzania kuchomoza juu uso wa dunia katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
Kwa Bandari za Tanzania, hii ni historia mpya ya mafanikio ingawa bado haipewi kipaumbele cha kuwekwa kwenye kumbukumbu rasmi na au hata kuutangazia ulimwengu na umma wa watanzania kuhusu mafanikio hayo ili kila Mtanzania anapozitazama bandari za nchi yake, ajipige kifua kujivuna.
Aliyeiweka Tanzania juu ya uso wa dunia ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), inayoshikiliwa kwa mikono miwili na Plasduce Mkeli Mbossa, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo ambaye naye historia ya mafanikio yaliyofikiwa; pamoja na kumtaja kwa mambo mengi, mawili yako dhahiri;

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Plasduce Mbossa.
Mosi, uwezo wa kusimamia maboresho ya Bandari za Tanzania; kazi aliyopewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa hakika ndiye kinara wa mafanikio haya na pili; kuuthibitishia umma wa watanzania kuwa Bandari za Tanzania hazijauzwa bali zinaendeshwa na kampuni binafsi chini ya usimamizi wa TPA.
Kwa mambo hayo mawili, Mbossa amefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuongeza tija katika shughuli za bandari, ajira kwa watanzania na kusimamia kwa mafanikio mageuzi ya kimfumo yaliyowezesha ongezeko la mapato tofauti kabisa na ilivyozushwa hapo awali kuwa Bandari za Tanzania zimeuzwa kwa wageni na kuwaacha watanzania mikono mitupu.
Hivi sasa, Tanzania ikiwa na nafasi yake ya kudumu katika ramani ya dunia kwenye sekta ya uchukuzi na usafirishaji, ni bandari tatu tu zilizowezesha hilo; nazo ni Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.

Bandari ya Dar es Salaam

Bandari ya Tanga
Bandari hizi ndizo zilizoguswa na maboresho yaliyofanywa TPA ya ukarabati wa magati, mifumo ya mawasiliano, kuongezwa kwa manjinika ya kisasa na mafunzo kwa watendaji.
Kwa waliofika katika bandari hizo tatu baada ya kufanyiwa maboresho makubwa na TPA watakuwa mashuhuda kuwa hivi sasa shughuli zinaendelea muda wote; mashine na mitambo inapishana muda wote kushusha na kupakia mizigo na kwa upande mwingine, watendaji wanapishana kuingia na kutoka kazini.
Katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara meli zinatia nanga na nyingine zikinyanyua kuondoka, manjinika zinafanya kazi mchana na usiku kupokea na kupakua mizigo kwa umakini mkubwa kwa kuwa mitambo na mifumo mingi ya kiutendaji ni ya kisasa.
Ripoti ya hivi karibuni ya utendaji wa bandari hizo tatu inaonyesha kuwa muda wa meli kutia nanga; kupakiwa na kupakuliwa kwa shehena umepungua kwa kiwango kikubwa tofauti na awali kabla ya bandari hizo kufanyiwa maboresho.
Ikiwa ni takribani miaka minne sasa ya mwendo wa mchaka mchaka wa mabadiliko ya kuondoa urasimu, upotevu wa mapato, tuhuma za rushwa na ubadhirifu, kucheleweshwa kwa mizigo na miundombinu chakavu katika bandari hizo, leo Tanzania inajivuna kuwa kitovu cha biashara ya usafirishaji kikanda.
Uamuzi wa Rais Dk. Samia wa Julai 4, 2022 kumteua Mbossa kuiongoza TPA kumerejesha imani kwamba Tanzania inaweza kusimamia vema rasilimali zake za kimkakakati licha ya kuwa katikati ya vita kali ya kiuchumi ianyoongozwa na mataifa yanayotaka kuvuna bure utajiri wa taifa hilo.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Plasduce Mbossa.
Akiwa kiongozi kijana, Mbossa ameweza kuiongoza TPA kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa injini ya kukusanya mapato lakini hasa ni kuuthibitishia umma wa watanzania na ulimwengu kuwa mageuzi ya kiuendeshaji yaliyofanywa kwenye Bandari za Tanzania ambayo yalitumiwa na maadui wa kiuchumi kama silaha ya kuishambulia serikali; yalilenga kuchochea mageuzi ya kimfumo ambayo matokeo yake ni mafanikio yanayopatikana sasa.
Wafuatiliaji wa mambo wanaeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana kwenye Bandari za Tanzania baada ya Mbossa kuteuliwa kushika usukani wa kuzisimamia yalichochewa na vipaumbele alivyoingia navyo ambavyo ni mageuzi ya mamlaka, kuimarisha ukaguzi, kusimika mifumo ya ndani ya udhibiti, kuingiza uwazi katika manunuzi na kusimamia ukusanyaji wa mapato.
Wanataja pia kusimamia uimarishaji matumizi ya teknolojia kwenye sekta zote na hasa kusomana kwa mifumo inayoshughulikia shehena, utendaji wa wafanya kazi wote na kuzindua jukwaa shirikishi kwa ajili ya upokeaji mizigo, uendeshaji wa bandari na mapato hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa mwingiliano wa moja kwa moja kati ya watu.
Yeye mwenyewe amepata kukaririwa akiwaeleza wadau wa usafirishaji jijini Dar es Salaam katika moja ya mikutano iliyowakutanisha kuwa hatua alizochukua baada ya kukabidhiwa hatamu za uongozi TPA, zilidhibiti vitendo vya rushwa na kuongeza ufanisi kwa kiwango kikubwa.
.
