Monday, December 23, 2024
spot_img

USHAHIDI TUHUMA ZA NAIBU WAZIRI MNYETI KIELELEZO KINACHOISHI

RIPOTI MAALUMU (4)

CHARLES MULLINDA

MASHAHIDI 12 waliohojiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyochunguza tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti wakati akiwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Manyara ni kielelezo kinachoishi cha matendo ya baadhi ya viongozi tulionao.

Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yenye maelezo ya maofisa wa polisi, Wakili wa Serikali Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, watendaji wa serikali, wananchi ambao katika ripoti hiyo ni mlalamikaji Dk. Hamis Kibola na hasimu wake kibiashara, Saleh Al Amry pamoja na Naibu Waziri Mnyeti kuhusu uzingatiaji wa maadili ya uongozi na kuheshimu Katiba ya Tanzania ni rejea inayopaswa kutumika sasa na huko tuendako kufanya tathmini ya kile kinachohubiriwa mdomoni na baadhi ya viongozi wetu kama ndicho wanachokiishi. HII NI RIPOTI MAALUMU.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mathew Mwaimu

Juni 28, 2021, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyokuwa ikichunguza tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka alizokuwa akituhumiwa nazo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, sasa ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ilimuhoji ambaye kwenye ripoti hiyo anatambulishwa kama Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Said Athumani Mabiye.

Mabiye anakaririwa kwenye ripoti kueleza kuwa Dk. Kibola alizuiwa kuingia kwenye kitalu chake cha uwindaji kwa amri ya Mnyeti iliyotekelezwa na Afisa Mtendaji Kata ya Emboreet, Belinda Sumari. Belinda aliondolewa Kata ya Emboreet akapelekwa Kata ya Loibosoit baada ya taarifa zake kumfikia Joseph Mkirikiti ambaye alichukua nafasi ya Mnyeti.  

Mabiye aliiambia Tume kuwa alimuita aliyekuwa Katibu wa Mnyeti, Ibrahim Mbogo aeleze anachokifahamu kuhusu suala hilo kwani yeye alikuwa halifahamu kwa undani.

Ibrahim Mbogo, yeye alihojiwa na Tume Juni 28, 2921 ambapo alieleza kuwa ingawa alikuwa Katibu wa Mnyeti lakini hakufahamu chochote kuhusu mgogoro huo kwa sababu Mnyeti hakumshirikisha bali alitoa maelekezo moja kwa moja kwa Belinda.

Alikana kuandika barua ya zuio kwa Dk, Kibola kuingia kwenye kitalu chake na alikana pia kuona barua ya malalamiko ya wananchi dhidi ya ujangili kama ilivyoelezwa na Mnyeti mbele ya Tume.

Peter Ngasa ni Wakili wa Serikali Ofisi ya Mashtaka ya Taifa Mkoa wa Manyara aliyefika mbele ya Tume Juni 28, 2021 kutoa ushahidi wake na alieleza kuwa alipata taarifa kuwa Dk. Kibola ana kesi ya uhujumu uchumi.

Kwamba Dk. Kibola na wenzake nane walikuwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 11/2020 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara iliyofunguliwa kutokana na taarifa za uchunguzi wa kamati ya Mnyeti na kwamba upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa ukiendelea.

Tume ilimuhoji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, ACP Mareson Mwakyoma Juni 28, 2021 aliyesema kuwa kwa mara ya kwanza alikutana na Dk. Kibola, Machi 2020 kwenye kikao kilichoitishwa na RC Mkirikiti na kwamba katika kikao hicho Dk. Kibola alilalamika kukamatwa na watu wasiokuwa na mamlaka kisheria.

Dk. Hamis Kibola

Ripoti inamkariri Kamanda Mwakyoma akieleza kuwa Dk. Kibola na wawindaji wengine walihoji watendaji wa kata kuwa na nguvu za kukamata watu wenye vibali halali vya uwindaji.

Alikiri ofisi yake kushiriki uchunguzi wa uwindaji haramu kwenye kitalu cha Dk. Kibola na ripoti kupelekwa kwa Mnyeti ili achukue hatua na kwamba ni kweli walimkamata Dk. Kibola.

Ripoti inaendelea kumkariri Kamanda Mwakyoma akishangaa kukithiri kwa matukio ya ukamataji wamiliki wa vitalu vya uwindaji na yalikuwa maoni mbele ya Tume kuwa ukamataji huo ulikuwa na malengo binafsi na si ya serikali.

Siku iliyofuata, Juni 29, 2021 ilikuwa zamu ya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Simanjiro, SSP Juma Majata ambaye maelezo yake kwenye ripoti yanaonyesha kuwa Dk. Kibola alikamatwa kwa tuhuma za kuhatarisha amani na kwamba amri ya kukamatwa kwake ilitokana na uchunguzi uliokuwa ukimuhusisha na uwindaji haramu.

ā€˜Alieleza kuwa uchunguzi huo ulikuwa ukifanywa na kamati iliyoundwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Alexander Mnyeti pamoja na Kikosi cha Taifa dhidi ya ujangili,ā€™ inasomeka ripoti.

SSP Juma anakaririwa zaidi kwenye ripoti kuwa Dk. Kibola alikaidi amri ya Belinda ya kutoingia kitaluni kwake kupisha uchunguzi na alikamatwa na mgambo waliokuwa chini ya uongozi wa Belinda kwa maelekezo ya Mnyeti ambaye alikuwa na mamlaka ya kuamuru mtu kukamatwa anapotenda kosa la jinai na kuwekwa mahabusu kwa saa 48.

ā€˜Baada ya mlalamikaji kukaa mahabusu kwa siku mbili, SSP Juma aliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Manyara kabla ya kuachiwa kwa kujidhamini mwenyewe lakini alimweleza akipata maelekezo mengine atamuita.

Belinda Sumari

Tume ilimuhoji aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi siku ya Julai Mosi, 2021 aliyeeleza kuwa hakupata maelekezo yoyote kutoka kwa mkuu wake wa kazi kuhusu suala la Dk. Kibola zaidi ya kuelezwa kwa mdomo na Belinda kuwa ameelekezwa na Mnyeti kumzuia kuingia kwenye kitalu chake.

Myenzi aliimbia Tume kuwa hakupewa barua yoyote ya kumzuia Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu na yeye Dk. Kibola hakuwahi kufikisha malalamiko kwake kuhusu kuzuiwa kuingia kwenye kitalu chake wala kukamatwa.

Ripoti inasema Myenzi alipigiwa simu na Belinda kumueleza kuwa amepewa maagizo na Mnyeti kupeleka mgambo wa kulinda kitalu cha Dk. Kibola na kumzuia kuingia na alikiri kuufahamu mgogoro kati ya Dk. Kibola na Saleh Al Amry na pia alifahamu kuhusu kamati ya Mnyeti na Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuzuia Ujangili.

Kwamba mapendeko ya kamati ya Mnyeti na Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuzuia Ujangili ndiyo yaliyotumika kufungua kesi iliyomkuta na hatia Gerald Kashiro aliyehukumu kwenda jela miaka 30 kwa kosa la ujangili.

Afisa Tarafa ya Emboreet, Chausiku Baha alifika mbele ya Tume kuhojiwa Juni 30, 2021 naye alieleza kuwa Mnyeti ndiye aliyeagiza kukamatwa kwa Dk. Kibola na ya kuwa kwa ufahamu wake, matatizo yalianza baada ya Dk. Kibola kutoelewana na mshirika wake wa biashara, Saleh Salum Al Amry.

ACP J. Mwafulango, Afisa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha yeye anakaririwa na Ripoti ya Tume kuwa aliitwa na Mnyeti kuelezwa kuhusu mgogoro baina ya Dk. Kibola na Al Amry na kwamba wawili hao walikuwa wanafanya uwindaji haramu.

Akiwa mbele ya Tume Julai Mosi, 2021 alisema Mnyeti alitoa agizo la kufungwa kwa kitalu cha Dk. Kibola lakini yeye alimshauri asikifunge badala yake aunde kamati ya kuchunguza tuhuma hizo ili kubaini ukweli.

ā€˜Mkuu wa Mkoa alikubali ndipo aliunda kamati iliyokuwa na wajumbe nane, Ofisi yake ilimteua SP Said Jafari Mchaki kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo iliyokabidhi taarifa yake kwa Mnyeti baada ya kumaliza kazi.

Siku hiyo hiyo ya Julai Mosi, 2021, Tume ilimuhoji SP Mchaki ambaye ripoti inaonyesha alieleza kuwa kamati iliyoundwa na Mnyeti ilipewa kazi ya kuchunguza tuhuma zilizokuwa zikimkabili Dk. Kibola za kujihusisha na uwindaji haramu na ilifanya kazi kwa muda wiki mbili.

Aliwataja mbele ya Tume wajumbe wa kamati hiyo kuwa waliteuliwa kutoka Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na uchunguzi wake ulibaini Dk. Kibola alikuwa akiazima na kutumia silaha kwa watu binafsi bila kufuata utaratibu, alikuwa anawinda wanyama wasioruhusiwa na haorodheshi wanyama waliotajwa kwenye vibali vya uwindaji.

Mapendekezo ya kamati ya Mnyeti ambayo Tume imeyaweka kwenye ripoti yake ni watuhumiwa kufikishwa mahakamani, TRA kuchukua hatua stahiki dhidi ya watuhumiwa kwa makosa ya kukwepa kulipa kodi na watumishi waliohusika na uwindaji haramu kuchukuliwa hatua za kisheria.

ITAENDELEA ā€¦.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya