RIPOTI MAALUMU (2)
CHARLES MULLINDA
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti ni mtovu wa maadili, anakiuka haki za binadamu na utawala bora na mvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Hayo ni baadhi ya aliyokutwa nayo na kuandikwa kwenye Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyochunguza tuhuma za matumizi mabaya ya Madaraka wakati akiwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Manyara; tuhuma hizo zilifikishwa mbele ya Tume na Dk. Hamisi Kibola, mwaka 2021.
Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inamuanika Mnyeti, ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kama mtu aliyekwishayapa kisogo maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye Oktoba 3, 2022 akiwa Ikulu, Dar es Salaam alisisitiza utii wa Katiba.
Aidha, April 2, 2022 akiwa Ikulu ya Chamwino, Rais Samia alizungumza kuhusu maadili ya utumishi wa umma, alisema; hali ya utumishi wa umma siyo nzuri sana ingawa mabadiliko yaliyofanywa na Serilali ya Awamu ya Tano yalikuwa yakisifiwa kukuza heshima kwenye utumishi wa umma. HII NI RIPOTI MAALUMU.
Rais Samia Suluhu Hassan
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilifanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwa Mnyeti, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, chini ya Mamlaka iliyo nayo kikatiba yanayotajwa kwenye Ibara ya 130 (I) (c) (f) na (g) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ikisomwa pamoja na vifungu vya 6 (1) (c) (f) na (g) , 11 (I) (b) (I) na 22 (5) (a) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, sura ya 391.
Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mathew Mwaimu inasema uchunguzi wake dhidi ya tuhuma za Mnyeti ulibaini kuwa akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, alimuamuru Mtendaji Kata ya Emboreet, Belinda Sumari kumkamata Dk. Kibola bila kufuata utaratibu kisha kumuweka mahabusu katika Kituo cha Orkasumeti, Simanjiro kwa muda wa siku mbili kwa sababu ya kuhatarisha amani.
Awali mwezi Disemba 19, 2019, Dk. Kibola alikamatwa na kikosi kazi kilichoundwa na Waziri wa Maliasili na Utalii akiwa Mkoa wa Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoani Arusha ambako aliwekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Utalii hadi Disemba 25, 2019 alipoachiwa kwa kijidhamini mwenyewe bila kufikishwa mahakamani.
Inasema kitendo cha kukamatwa kwa Dk. Kibola kisha kujidhamini mwenyewe kinaonesha makosa aliyokuwa akituhumiwa nayo hayakuwa na ushahidi na kwamba ukamataji uliofanyika haukufuata utaratibu kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20.
Ripoti ya Tume inaonyesha kuwa Mnyeti alivunja haki za binadamu kwa kumzuia Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu chake cha uwindaji anachokimiliki kisheria na akiwa na vibali vya mamlaka zinazohusika na usimamizi wa shughuli za uwindaji wa wanyamapori.
Jaji Methew Mwaimu
Kwamba Mnyeti alitenda kinyume na Ibara ya 24 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi ya mali yake kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu haki ya uhuru wa mtu binafsi na haki ya kufanya kazi, ripoti ya Tume inasomeka hivi; ‘kitendo cha mlalamikaji kukamatwa kwa agizo la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara (Mnyeti) na kuwekwa mahabusu kwa siku saba katika Kituo cha Polisi cha Utalii, Arusha na siku mbili Kituo cha Polisi Orkasumet, Simanjiro bila kufikishwa mahakamani kulimnyima mlalamikaji haki ya kuwa huru kwa mujibu wa Ibara ya 17 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
‘Zuio alilowekewa mlalamikaji la miezi nane lilimzuia kufanya shughuli za uwindaji katika kitalu anachomiliki kisheria na kulipa vibali vyote, kulimnyima haki yake ya kufanya kazi kama ilivyoelezwa kwenye Ibara ya 22 (1) ya Katiba ya Jamhuti ya Muungano wa Tanzania ya mwmaka 1977.’
Ripoti inamtaja pia Mnyeti kama mtu asiyekuwa na maadili kwa kutoa taarifa zisizokuwa na uthibitisho kwa Tume ambayo wakati ikimuhoji alisema aliweka zuio kwa maandishi kwa Dk. Kibola kutoingia kwenye kitalu chake cha uwindaji lakini kinyume chake, Tume ilibaini kuwa hakusema ukweli kwa sababu hakukuwa na maandishi, bali aliagiza kwa mdomo.
Aidha, Tume ilibaini pia kuwa Mnyeti alitoa taarifa zisizo za kweli kwa Tume kwa kueleza kuwa alipokea barua ya malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kuwepo uwindaji haramu kwenye kitalu cha Kampuni ya HSK Safaris Ltd lakini uchunguzi wa Tume ulibaini hapakuwa na barua yoyote ya malalamiko iliyowasilishwa na wananchi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Dk. Hamis Kibola
Mnyeti anatajwa pia kwenye harufu ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ambapo ripoti ya Tume inaeleza kuwa hilo ni kwa sababu ya uwepo wa uhusiano kati yake na Saleh Salum Al Amry ambaye kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alichimba visima vya maji jimbo la Misungwi ambalo Mnyeti ni mbunge wake.
Ripoti inamtaja Mnyeti kama mkiukaji wa misingi ya utawala wa sheria kwa kutoa agizo bila kufuata utaratibu kwani yeye kama mkuu wa mkoa hakuwa na mamlaka ya kumzuia Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu anachokimiliki kwa mujibu wa sheria isipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye amepewa mamlaka hayo kwenye kifungu cha 38 (12) na (15) cha Sheria ya Usimamizi Wanyamapori, sura ya 283.
Mnyeti anatajwa pia kwa kutozingatia ushirikishwaji kwenye uamuzi wa kuweka zuio la kufanyika shughuli zozote kwenye kitalu cha Dk. Kibola ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA zenye mamlaka na dhamana ya masuala ya uhifadhi wa wananyamapori aliziweka kando.
Kuhusu uwazi, ripoti inasomeka hivi; ‘katika uchunguzi huu hakuna uwazi wa nani hasa alipeleka taarifa kwa mkuu wa mkoa kuhusu tuhuma za ujangili dhidi ya kampuni ya mlalamikaji.
‘Pia baada ya kamati ya mkuu wa mkoa kumaliza majukumu yake, mlalamikaji ambaye ni mtuhumiwa katika uchunguzi hakujulishwa matokeo ya uchunguzi huo.’
Alexander Mnyeti
Na kuhusu ufanisi na tija, ripoti inasomeka; ‘Kamai ya mkuu wa mkoa haikuwa na tija kwa kuwa taarifa yake haikuwafikia wadau ambao kisheria walipaswa kupewa taarifa hiyo.
‘Aidha, Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA walitoa vibali vya uwindaji kwa mlalamikaji ili kuingizia serikali mapato kwa kulipa kodi. Kuweka zuio kulisababisha mteja halali kushindwa kupata mapato na kumwezesha kulipa kodi serikalini na hivyo kuikosesha serikali mapato kwa kipindi hicho.’
Uwajibikaji, ripoti inasomeka; ‘kitendo cha mkuu wa mkoa na afisa mtendaji wa kata kutojibu barua za terehe 11/3/2020 na ile ya tarehe 27/4/2020 walizoandikiwa na mlalamikaji pamoja na kitendo cha mkuu wa mkoa kukataa kuonana na mlalamikaji ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika eneo la uwajibikaji kwa viongozi wa umma.
ITAENDELEA KESHO.