RIPOTI MAALUMU (5)
CHARLES MULLINDA
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, wakati ikichunguza tuhuma za Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti za matumizi mabaya ya madaraka na kukiuka misingi ya utawala bora alipokuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Manyara, ilielezwa kuwa uamuzi wake (Mnyeti) wa kumzuia Dk. Hamis Kibola kuingia kwenye kitalu chake, hautambuliki.
Tanzania PANORAMA Blog ambayo imeiona ripoti hiyo, imezingatia uzito wake na kwa kuiishi kauli za Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuanzishwa kwa Tume hiyo na majukumu yake yanayotambulika kikatiba inaripoti kwa umma uchunguzi na uamuzi wake. HII NI RIPOTI MAALUMU.
Rais Samia Suluhu Hassan
EMMANUEL Pius, Mhifadhi Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Kanda ya Kaskazini alihojiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Julai 3, 2021 na bila kusita alieleza kuwa TAWA haitambui zuio lililowekwa na Mnyeti kwa Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu chake cha uwindaji.
Ripoti ya Tume inasomeka hivi; āEmmanuel Pius aliieleza Tume kuwa TAWA ilikuwa inamtambua Dk. Hamis Kibola kama mdau wao aliyekuwa anamiliki vitalu viwili kupitia Kampuni ya HSK Safaris Ltd.
āVitalu hivyo ni kitalu cha Simanjiro West na kitalu cha Ngalambe/ Tapika kilichopo Rufiji mkoani Pwani.
āEmmanuel alieleza kwamba kibali cha uwindaji hutolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii kupitia TAWA na kwamba kwa mujibu wa sheria, hakuna mamlaka nyingine yenye uwezo wa kuweka zuio isipokuwa waziri mwenye dhamana ya Maliasili na utalii.
āAlisisitiza kwamba TAWA haikuwahi kutoa maagizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara kuweka zuio kwa Hamis Kibola na wala haitambui zuio lililowekwa na Mkuu wa Mkoa kwa mteja wao.
āVile vile alieleza kushangazwa na uamuzi wa Dk. Kibola kuwasilisha malalamiko Tume wakati hakuwahi kupeleka lalamiko kwao la kuzuiwa kuingia kitaluni na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa,ā inasomeka ripoti.
Ripoti ya Tume inamkariri zaidi Pius kuwa; deni la Dola za Marekani 88,630 alilokuwa anadaiwa mlalamikaji na TAWA lilikuwa linamnyima fursa ya kupata kibali cha uwindaji lakini aliingia makubaliano na TAWA ya kulipa deni hilo kwa awamu tatu.
Kwamba TAWA ilimuandikia barua mlalamikaji ya kumpa msamaha ili aweze kulipa baadhi ya gharama na awamu ya kwanza alilipa Dola za Marekani 25,000 ndipo aliporuhusiwa kwa barua iliyoandikwa na TAWA Januari 13, 2021.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mathew Mwaimu
Kabla ya hapo, Julai Mosi, 2021 Tume ilikuwa imesikiliza maelezo ya Saleh Salum Al Amry ambaye ripoti inamkariri kuwa aliingia makubaliano na mlalamikaji kuendesha shughuli za uwindaji katika kitalu cha Simanjiro West ambapo mlalamikaji alikubali kutoa kitalu na Al Amry alikubali kufanya ujenzi, kutoa silaha na magari.
Taarifa ya Tume inaeleza kuwa Al Amry alieleza kuwa alitekeleza majukumu yake lakini kwa miaka mitatu hawakupata faida kwa sababu mshirika wake alikuwa hamshirikishi katika kazi na alikuwa hana haki za akaunti ya kampuni.
āAlieleza pia kuwa wakati wanaendelea na ushirika huo, mlalamikaji aliingia makubaliano na Kampuni ya Franklin inayomilikiwa na Abdulnaset kufanya naye biashara.
āAlisema pia kuwa mlalamikaji alimkana mbele ya polisi kuwa walikuwa wanafanya biashara pamoja na kudai hana mkataba naye. Hii ilisababisha Saleh awekwe mahabusu kwa kosa la kughushi mkataba na siku ya pili alitolewa kwa dhamana.
āHata hivyo, kwa maelezo yake, baada ya miezi miwili polisi walimjulisha kuwa mkataba wake ni halali ndipo alipofungua kesi ya madai dhidi ya Dk. Kibola,ā inasomeka ripoti.
Inaendelea kuwa Saleh anakumbuka kuitwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara alikoelezwa kampuni yao ya HSK Safaris Ltd inajihusisha na ujangili na alihojiwa na Kikosi Kazi kwa tuhuma za kuiba silaha kabla ya kuwekwa mahabusu kwa siku nne kisha kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara.
ITAENDELEA