RIPOTA PANORAMA,
DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetoa rai kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeleza mafanikio makubwa iliyopata katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Pia, kamati hiyo imeipongeza serikali kwa kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza juzi jijini Dodoma kwenye kikao cha kamati hiyo, wizara na taasisi zilizo chini yake, Mwenyekiti wa kamati, Thimotheo Mzava alisema mafanikio yaliyofikiwa na wizara pamoja na taasisi zake kwa miaka minne iliyopita ni ya kupigiwa mfano.
Baadhi ya wajumbe waliopata fusra ya kuzungumza kwenye kikao hicho ambacho kilikuwa mahususi kwa ajili ya wajumbe wa kamati kujifunza muundo na majukumu ya wizara na taasisi zake, walisema wapo tayari kushirikiana na wizara kuendeleza uhifadhi ili kizazi kijacho kinufaike na rasilimali hiyo muhimu.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao hicho, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji alisema serikali itaendelea kuwa sikivu na kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuendeleza sekta ya uhifadhi na utalii ili kuwanufaisha wananchi wote.

Taasisi zilizowasilisha taarifa zake katika kikao hicho kwa niaba ya Waziri Dk. Kijaji ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA) na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT).
