RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amezitaka Halmashauri za Jiji kote nchini kuondoa masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanaohitaji ili wananchi wengi zaidi wamufaike.
Akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Agnesta Kaiza, Alhamis, Januari 29, 2026 aliyehoji kuhusu utaratibu wa upatikanaji wa mikopo hiyo, Waziri Mkuu Dk. Nchemba alisema wananchi wanaweza kutumia Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kupata mikopo hiyo.
Alisema wale ambao hawana vitambulisho vya Taifa wanaweza kutumia barua za utambulisho kutoka ofisi za Serikali za Mitaa au Vijiji.

Mama ntilie wakiwa kazini. Kundi hili la wafanyabiashara wadogo wa chakula ni miongoni mwa wanaopaswa kunufaika na mikopo ya asilimia 10 (Picha ya mtandao)
Waziri Mkuu Dk. Nchemba alisema mikopo hiyo hutolewa kwa makundi maalum ya wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4) na wenye ulemavu (asilimia 2) ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na alisisitiza kuwa hakuna haja ya kuwepo masharti magumu,
Alisema ndani ya siku 100, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha ongezeko la Shilingi bilioni 200 katika mfuko wa mikopo ili kuongeza wigo wa mikopo kwa wananchi wote.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anamaanisha katika suala la kuwawezesha vijana, wanawake, na ndugu zetu kutoka makundi maalum. Ndiyo maana kaongeza Shilingi bilioni 200 katika siku 100 baada ya kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema
Alisisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya jitihada za serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima na kuimarisha miundombinu ya huduma za jamii.
