RIPOTA PANORAMA
KAZI mahususi ya kuboresha miundombinu ya Bandari za Tanzania iliyofanywa na serikali ya awamu ya sita imezaa matunda.
Taarifa ya serikali iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa alipofanya ziara katika Bandari ya Dar ea Salaam, inaeleza kuwa kazi hiyo mahususi iliyofanywa na serikali imeongeza mapato ya serikali, imeboresha ufanisi wa huduma na imevutia watumiaji wengi kutoka nchi jirani.
Akizungumza bandarini hapo, Msigwa ambaye pia ni msemaji mkuu wa serikali aliitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kushika nambari moja kwa kutumia Bandari za Tanzania.
Msigwa alisema uimarishaji wa Bandari za Tanzania hususan Bandari ya Dar es Salaam, kumeimarisha nafasi ya Tanzania kama lango kuu la biashara kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Akilitumia jukwaa hilo kuelezea kazi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na mafanikio yaliyopatikana katika siku 100 alizokaa ofisini kwa awamu ya pili ya uongozi wake, Msigwa alisema uwekezaji uliofanywa na serikali katika Bandari za Tanzania umechochea ukuaji wa uchumi, umepunguza muda wa meli kukaa bandarini na umeongeza ushindani wa Bandari za Tanzania kikanda na kimataifa.

Maafisa wa TPA wakimsikiliza Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, (hayupo pichani) akielezea mafanikio yaliyofikiwa na serikali katika kipindi cha siku 100.
Akirejea takwimu rasmi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) za mwaka wa fedha 2024/2025, alisema Bandari za Tanzania zimehudumia shehena tani 5,995,293 za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Shehena tani 3,510,706 za Zambia, shehena tani 1,724,370 za Rwanda, shehena tani 675,200 za Malawi, shehena tani 425, 774 za Burundi, shehena tani 185, 625 za Uganda, shehena tani 61,308 za Zimbabwe na shehena za nchi nyingine tani 38, 512.
Aidha, Msigwa alirejea tena kuutarifu umma wa watanzania kuwa TPA ilisaini mkataba wa uendeshaji bandari na Kampuni za DP World Dar es Salaam Limited na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) kwa ajili ya kuimarisha ufanisi.
Alisema, hadi Juni 2025 Kampuni ya DP World iliwekeza Shilingi bil 214.2 kwenye mitambo, miundombinu na TEHEMA na Kampuni ya TEAGTL iliwekeza Shilingi bil. 410.4 katika ukarabari wa gati, ununuzi wa mitambo na mifumo ya kisasa katika kipindi kama hicho.
“Uwekezaji umeongeza shehena hadi kufikia tani milioni 27.7 mwaka 2024/2025 – ongezeko la asilimia 17 – na tani milioni 16.7 kati ya Julai hadi Desemba 2025 – ongezeko la asilimia 30.

“Muda wa kuhudumia meli za makasha umepungua kutoka siku 30 hadi siku sita tu, ajira 764 za moja kwa moja zimezalishwa na makusanyo ya kodi ya forodha yamefikia Shilingi tril. 12.33 sawa na ongezeko la asilimia 17,” alisema Msigwa.
Aidha, Msigwa aliitaja miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kuwa ujenzi wa gati na matanki 15 ya mafuta, uboreshaji wa gati la Malindi na reli ndani ya bandari itakayoongeza uwezo hadi TEUs 480,000 kwa mwaka.
Alisema maboresho yatafanyijka pia katika bandari nyingine ikiwemo Bandari ya Mgao Mtwara, Kemondo Bukoba, Mwanza Kaskazini, Kigoma, Tanga na Mbamba bay.
