MHINA SEMWENDA
MAWAZIRI na katibu wakuu wametakiwa kusimamia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ili kukabiliana ipasavyo na changamoto zinazowakabili wananchi.
Agizo hilo lilitolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba alipokuwa akifungua kikao cha mawaziri na katibu wakuu wa wizara za kisekta kilichoketi mahususi kujadili fursa za ajira ndani na nje ya nchi.
Alisema wizara zinazohusika na ajira zisimamie kikamilifu utekelezaji wa sheria inayoelekeza kazi zinazoweza kufanywa na watanzania zisifanywe na wageni isipokuwa kazi zinazohitaji utaalamu ambao watanzania hawana.
Aidha, Dk. Nchemba alikemea tabia ya baadhi ya wenye nyumba kupangisha raia mmoja wa kigeni na kumruhusu kupangisha watu wengine ndani ya nyumba hiyo jambo ambalo ni hatari kiusalama na halina tija kibiashara.
Agizo na onyo la Waziri Mkuu Nchemba yanalenga kuongeza fursa za ajira kwa watanzania baada ya kuwepo wimbi la raia wa kigeni kufanya kazi au biashara zinazoweza kufanywa na watanzania.
“Kazi zinazoweza kufanywa na watanzania ziachwe wafanye, si kuruhusu wageni wafanye. Tusioneane aibu, kama tumefungua milango au kulegeza wataalamu wafuatilie. Wageni wafanye kazi za kitaalamu ambazo nchi ina uhaba wa wataalamu,” alisema.
Dk. Nchemba alitoa wito kwa wananchi kuwa na wivu na nchi yao
“Watanzania tuwe na wivu na nchi yetu, mfano mtu anamkodishia nyumba mgeni kwa Dola 5,000 kwa mwaka na kisha mgeni huyo anawaleta wenzake 60 na anawakodisha dola 500 hapo Mtanzania anapata hasara, hii si sawa hata kwa usalama.”
