Wadau wa usafi wa mazingira katika Jiji la Arusha, wakiwemo Maafisa Afya kutoka kata zote 25, wakandarasi wa huduma ya uzoaji taka pamoja na mawakala wa ukamataji wa wachafuzi wa mazingira, wamekutana katika kikao kazi cha kuimarisha usafi wa mazingira ili kuhakikisha jiji linakuwa safi, salama na lenye kuvutia wakati wote, hususan kuelekea michuano ya AFCON 2027.
Akizungumza Aprili mosi, 2026, Meya wa jiji hilo, Maxmillian Iranqhe amesema lengo la kikao hicho ni kuhakikisha jiji linakuwa safi ili kuendana na hadhi ya kuwa makao makuu ya taasisi mbalimbali za kimataifa, zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Shirika la Posta Afrika (PAPU).
Arusha ni mwenyeji wa mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa hivyo ni muhimu kudumisha usafi wa mazingira kwa ajili ya kuvutia wageni na kulinda heshima ya jiji, na ukusanyaji wa taka ufanyike kwa wakati na kwa ufanisi ili kuhakikisha maeneo yote ya jiji yanabaki safi muda wote,” amesema Iranqhe.





