
SEKTA ya Utalii Tanzania imeng’ara katika viwango vya kimataifa kwa ongezeko la watalii na mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism) ya mwaka 2024 iliyotolewa Desemba mwaka jana nchini Uswisi, Sekta ya Utalii Tanzania imeshika nafasi ya sita duniani kwa ongezeko la watalii wengi wa kimataifa.
Mafanikio haya makubwa kwa Sekta ya Utalii Tanzania kushika nafasi za kilele duniani yamekuja miaka mitatu baada ya Raisi Dk. Samia Suluhu Hassan kuigiza filamu ya kihistoria ya The Royal Tour.
Raisi Dk. Samia ambaye kwenye filamu hiyo inayofahamika kwa Lugha ya Kiswahili kama ziara ya kifalme, ameigiza kama mhusika mkuu; lengo lake lilikuwa kuuonyesha ulimwengu uzuri wa Tanzania kwa kuangazia uzuri wa Hifadhi za Taifa zilizopo Tanzania Bara, fukwe nzuri za Zanzibar, utamaduni na watu wa Tanzania.
Akitekeleza azma yake aliyoitangaza alipokuwa akiingia madarakani kuwa ataendelea kusimamia misingi ya Taifa na kuyahakikishia mataifa ya nje kuwa Tanzania ni mahali salama pa kutembelea ikiwa na fursa lukuki za uhakika za uwekezaji katika sekta ya Maliasili na Utalii.

Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan
Raisi Dk. Samia alimteua Musa Juma Kuji kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambaye amefanikiwa kulivusha kwenye mtikisiko wa mvua za Eli nino zilizotikisa sehemu nyingi duniani na pia ameliwezesha shirika hilo kuvuka malengo yaliyowekwa na Serikali kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii yenye takwimu za mwenendo wa utalii na watalii duniani kuanzia mwezi Januari hadi Septemba, 2024 inaonyesha Tanzania imepanda kwa nafasi tatu kwa ongezeko la watalii wa kimataifa kutoka nafasi ya tisa hadi ya sita.
Kwa upande wa Ukanda wa Afrika na Mashariki ya Kati, Tanzania imeshika nafasi ya kwanza kwa Afrika kwa ongezeko la watalii wa kimataifa ikiiacha nyuma Morocco ambayo ilikuwa ikishikilia nafasi hiyo.



Na aidha, Tanzania imeshika nafasi ya tatu kwa ukanda wa Afrika na Mashariki ya Kati ikipata asilimia 49 ya ongezeko la watalii ikiwa imetanguliwa na nchi za Qatar, Albania, El Salvador, Saudi Arabia, Visiwa vya Virgin na Jamhuri ya Moldovas.
Ripoti inaangazia pia ongezeko la mapato ya Sekta ya Utalii kwa kila nchi ambapo Tanzania imeshika nafasi ya kwanza kwa Ukanda wa Afrika ikifuatiwa na Moroko.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii zinaonyesha kuwa mapato yatokanayo na utalii kwa Tanzania yameongezeaka kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na kipindi kabla ya ugonjwa wa Uviko 19.
Takwimu za karibuni zilizotolewa na shirika hilo zinaonyesha kuwa kati ya mwezi Agosti na Septemba 2024, Tanzania imeshika nafasi ya saba kwa mapato yaliyopatikana kwa Shilingi za Tanzania na Dola ya Marekani kutokana na utalii ikitanguliwa na nchi za Serbia, Pakistani, Romania, Japan, Ureno na Nicaragua.
