RIPOTA PANORAMA
MARA tu unapokanyaga ardhi ya Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa, miguu yako inakuwa imeelekea nchi mbili za Uganda na Rwanda na macho yako yanakuwa yanatizama mambo yote yanayoendelea ndani ya sehemu ya nchi hizo.
Hili ni moja ya maajabu yaliyo kwenye hifadhi hii iliyoanzishwa rasmi Julai 5, 2019, kwa tangazo la Serikali namba 509 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 294 baada ya kupandishwa hadhi kwa Pori la Akiba la Ibanda.
Hifadhi ya Ibanda – Kyerwa ipo Kaskazini Magharibu mwa Tanzania na imepambwa na mikunjo ya milima, mabonde, tambarare, mito ya muda na ya kudumu pamoja na ardhi oevu. Ni eneo linalovutia sana.

Kaimu Mkuu wa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Charles Ngendo
Kaimu Mkuu wa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Charles Ngendo amezungumzia uzuri na maajabu yaliyo kwenye hifadhi hiyo pamoja na hatua za makusudi za Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) za kutangaza hazina ya urithi wa historia ulio kwenye hifadhi hiyo.
“Ibanda – Kyerwa ndiyo hifadhi pekee hapa nchini ambayo eneo lake limepakana na nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Uganda na Rwanda. Watalii wanaofika hapa wanasema ukikanyaga Hifadhi ya Ibanda – Kyerwa unakuwa umekanyaga pia Uganda na Rwanda, wameibatiza hifadhi hii kuwa hifadhi ya miguu mitatu. Ni maajabu ya Mungu yaliyo Tanzania,” anasema.
Anasema mtalii akiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa anaweza kuona kwa karibu kabisa upande wa nchi ya Uganda na upande wa nchi Rwanda na hilo limekuwa likivutia watalii wengi kufika hifadhini hapo.

Mto Kagera
Ngendo anasema sehemu kubwa ya mpaka wa hifadhi na nchi za Uganda na Rwanda ni eneo la maji ya Mto Kagera ambao una historia ya kipekee na kwamba watalii wengi hutumia muda wao kufuatilia historia ya mto huo wenye simulizi nzito ya vita ya Uganda na Tanzania ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda.
Kama ilivyo katika baadhi ya hifadhi nyingine hapa nchini, Ngendo anasema Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa ni sehemu sahihi kwa wanafunzi kufanya ziara za kimasomo kwa sababu mbali na kujionea vivutio mbalimbali wanapata pia fursa ya kujifunza historia.
“Serikali imeweka mazingira mazuri sana kwa watalii wa ndani kuingia kwenye hifadhi, badala ya kuwaachia wageni peke yao kutoka mataifa ya mbali kuja kujifunza historia hapa, nawaarika vijana wetu na walimu wao kuja kufanya ziara za kimasoma hapa kwa sababu watapata muda wa kupumzika, kujionea vivutio vyetu na kujifunza historia, tupo tayari kuwapokea na tutawahudumia vizuri sana, hawatajuta hata kidogo,” anasema Ngendo.
Na hapo anaongezea kuwa Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa imepakana na Hifadhi ya Akagera ya nchini Rwanda kwa upande wa Kusini Magharibi.

Enel la misitu lililopo Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa.
Akizungumzia upekee wa hifadhi hiyo, Ngendo anasema Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa imepambwa na maeneo yenye uoto wa asili kuanzia nyika za miti ya migunga, milima na mabonde, mito na tambarare zinazoifanya iwe na mandhari nzuri ya kuvutia.
Anataja fursa anazoweza kupata mtalii akiwa ndani ya hifadhi hiyo yenye nyika ya savana, milima, mito, Mto Kagera na mabonde ambavyo vimejazwa wanyama wa aina mbalimbali, mtalii anaweza kujionea wanyama wa aina ya nyati, chui, viboko, swala, nyani na kima.
Katika Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa, mtalii anaweza kutalii kwa gari na au anaweza kutalii kwa kutembea kwa miguu ambapo huweza kuwa karibu zaidi na wanyama na kujifunza zaidi tabia ya maisha yao ya porini.
Anasema zipo njia mbalimbali zinazotumika kwa utalii wa kutembea kwa miguu ambapo mtalii huongozwa na askari wa hifadhi mwenye silaha kwa ajili ya kulinda usalama.

Tandala mdogo anayepatikana Hifadhi ya Taifa Ibanda – Kyerwa
Ngendo anasema ili kufika Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa, mtalii anaweza kutumia usafiri wa anga ambapo atatua Uwanja wa Ndege wa Bukoba na au anaweza kutua Uwanja wa Ndege ya Chato.
Baada ya kutua, mtalii atasafiri kwa gari umbali wa kilomita 221 kutoka Bukoba mjini hadi hifadhini na akiwa anatokea Chato atasafiri kwa barabara umbali wa kilomita 441 hadi eneo la Murongo na kuingia hifadhini. Katika safari hiyo kwa njia ya barabara mtalii atajionea maeneo ya utamaduni ya kabila la wanyambo, kilimo cha migomba, mashamba makubwa ya miwa na kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar.

Shamba la migomba linalopatikana Karagwe
Mbali na njia hiyo, pia mtalii anaweza kufika hifadhini akitokea upande wa Uganda kupitia mpaka wa kimataifa wa Murongo au Kikagari. Baada ya kuvuka eneo la mpaka, atasafiri kwa njia ya barabara umbali wa kilomita nne hadi kuingia makao makuu ya hifadhi ambayo yapo umbali wa kilomita tatu kutoka hifadhini.
Kuhusu hali ya hewa, Ngendo anasema kuna misimu miwili ya mvua; msimu wa mvua za vuli zinazoanza mwezi Oktoba hadi Novemba na msimu wa mvua za masika ambao ni wa mvua nyingi unaoanza mwezi Machi hadi Mei.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki
Ngendo anazungumzia pia upatikanaji wa huduma kwa watalii kuwa ni wa kuridhisha na hasa baada ya uongozi wa sasa wa Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA kuwekeza nguvu kubwa kwenye utoaji huduma bora kwa wageni.
Anawataja Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki na Kamishna wa Uhifadhi, Juma Kuji kama viongozi walioingia na mwelekeo unaolenga kuimarisha huduma kwa wageni ili kuzidi kuimarisha soko la utalii kwenye hifadhi changa zenye vivutio vya kipekee.

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Juma Kuji
Anasema msisitizo wa viongozi hao wa uboreshaji huduma kwa wageni kwenye eneo la hifadhi linalopokea mvua nyingi kwa wastani wa milimita 700 hadi 1000 kwa mwaka na wastani wa joto, ambao ni nyuzi joto 13 hadi 26, unalolifanya kuwa la ubaridi umewezesha upatikanaji huduma bora kwa wageni wanaotoka kwenye mazingira ya baridi na ya joto.
Ngendo anasema pamoja na jitihada za viongozi hao kuwa na matokeo chanya, bado ipo haja kwa Serikali kuwekeza nguvu zaidi kwenye ujenzi wa hoteli na maeneo ya chakula.
Anasema hivi sasa ipo hoteli moja; Ibanda Rumanyika Lodge iliyopo umbali wa kilomita tatu nje ya hifadhi yenye hadhi ya kuhudumia watalii kutoka nje ya nchi na kwa watalii wa ndani, zipo nyumba za kulala wageni maeneo ya Murongo zenye hadhi ya kati ambazo zina sifa ya kutoa huduma bora kwao.






