RIPOTA PANORAMA
BUNGE limeelezwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipaswa kujiuzulu wadhfa wake wa uwaziri mkuu kwa kushindwa kumudu majukumu yake.
Kauli kuwa Waziri Mkuu Majaliwa alipaswa kujiuzulu wadhfa wake ilitolewa Aprili 24, 2024 bungeni, Dodoma na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mbunge wa kisesa, Luhaga Mpina
Akichangia, Mpina alieleza msingi wa hoja yake kuwa ni kutotekelezwa kwa maagizo ya Waziri Mkuu Majaliwa aliyoyatoa Aprili 27, 2023 kuhusu oparesheni zinazofanywa na viongozi na watendaji wa taasisi za umma zinazokandamiza wananchi kiasi cha kuwasababishia ulemavu wa kudumu.
Mpina alisema Majaliwa alipaswa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa kuzingatia Ibara ya 51 (3) (e) ya Katiba kuhusu ukomo wa kushika madaraka ya nafasi ya Waziri Mkuu na Ibara ya 52 kuhusu kazi na mamlaka ya Waziri Mkuu.
Alisema mawaziri na watendaji wa serikali waliopuuza maagizo ya Waziri Mkuu nao walipaswa kufukuzwa kazi na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwani dhana ya utawala bora inaelekeza uwajibikaji dhidi ya wananchi.
“Katika dhana ya utawala bora haiwezekani akakosekana mtu wa kuwajibika, leo damu za wananchi zinaendelea kumwagika, mateso ambayo wananchi wanayapata kuishi kama wakimbizi kwenye nchi yao, dhuluma na uonevu unaoendelea haiwezi kuwaacha salama wahusika,” alisema.

Wabunge wakiendelea na shughuli za Bunge katika Ukumbi wa Bunge, Dodoma
Mpina alisema Waziri Mkuu alitoa maagizo Aprili 27, 2023 na yeye alilalamika bungeni Mei 3, 2023 lakini wiki moja baadaye operesheni ziliendelea na hata baada ya mwongozo wa Spika wa Juni 28, 2023 lakini hadi Aprili, 2024 ikiwa ni mwaka mzima umepita operesheni zinafanyika bila kuwashirikisha wananchi na viongozi wa maeneo husika.
Alisema wananchi wanapigwa, wanateswa, wanajeruhiwa, wanasababishiwa ulemavu wa kudumu na kuuawa.
Mpina alisema wananchi wanapigwa faini kinyume cha sheria, wanavamiwa na kuharibiwa mazao yao na kunyang’anywa mifugo, mifugo inakamatwa na kuuzwa kiholela, inakosa matunzo na kufa ikiwa imeshikiliwa hifadhini.
Akiendelea kuchangia, alisema kamatakamata isiyozingatia sheria inaendelea ingawa alitoa ushahidi wenye vielelezo vya kujitosheleza vilivyothibitishwa na Ofisi ya Bunge kama alivyotakiwa na Spika wa Bunge kuhusu malalamiko yake lakini hakuna hatua zozote mahususi zilizochukuliwa na badala yake dhuluma na mauaji yanaendelea kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Alitoa mfano wa maeneo ya Meatu, Mbarali, Ngorongoro, Tarime na Kaliua ambako matukio ya aina hiyo yanatendeka na aliwataja wabunge wenzake ambao wamekuwa wakilalamikia matukio hayo kuwa ni Ester Matiko, Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Mara na Emmanuel Ole Shangai,Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro.

Hayati Edward Lowassa
Alisema Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alijiuzulu kwa makosa yaliyofanywa na watendaji walio chini yake kwa kumwandikia barua Rais wa wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliridhia kujiuzulu kwake.
Alimtaja pia Hayati Edward Ngoyayi Lowasa, aliyesema akiwa Waziri Mkuu alijiuzulu nafasi yake kwa tuhuma na mwingine aliyemtaja ni Dk. Emmanuel Nchimbi, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mawaziri wenzake sita walijiuzulu nyadhifa zao kwa madhila yaliyotokana na operesheni tokomeza.
Katika orodha hiyo ya viongozi waliopata kujiuzulu, alimtaja pia George Simbachawene ambaye alijiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Tawala za Mikoa sa Serikali za Mitaa (TAMISEMI) baada ya kutuhumiwa kuhusika kwenye mikataba ya madini akiwa Waziri wa Nishati na Madini.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko
Mpina alimtaja pia Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango aliyesema ameonyesha njia kuwa hawezi kuendelea kuwepo kwenye nafasi ambayo hawezi kutekeleza majukumu yake.
Mbali na hao, alimtaja pia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair ambaye alijiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu baada ya kubainika kuwa sababu za kuivamia na kuipiga Iraq (Casus belli) hazikuwa na ukweli kwani nchi hiyo haikuwa inamiliki silaha za maangamizi (WMD Trinity) kama ilivyokuwa imeelezwa awali.