ABBAS MWALIMU
0719258484
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Jumanne tarehe 27 Julai, 2021 aliwaapisha mabalozi wapya 13 kati ya 23 aliowateua mwezi Mei, mwaka huu, 2021.
Baadhi ya mabalozi hao watahudumu nchi kutokea ndani na wengine kama Balozi Hoyce Temu aliyepelekwa Geneva kuwa Naibu Mkuu wa Kituo wakipelekwa katika vituo (nchi) mbalimbali kuhudumu na baadhi wakisubiri taratibu za vituo kama alivyobainisha Mheshimiwa Rais Samia.
Mara baada ya kuwaapisha mabalozi hao, Rais Samia alizungumza na watanzania kupitia mabalozi hao.
Miongoni mwa mambo aliyozungumza Mheshimiwa Rais Samia katika hotuba yake ni diplomasia ya dijitali (Digital Diplomacy) akitumia neno ‘dunia ya sasa n dunia ya mtandao’, alizungumzia pia Diplomasia ya Umma ama Public Diplomacy, Diplomasia ya Afya (Health/Medical Diplomacy), waishio nje (Diaspora), uwekezaji kwa watu (Human Assets Index) na kujitegemea (Self Reliance).
Kwa bahati nzuri nilipata kuyaandikia masuala haya yote katika nyakati tofauti na hivyo leo ninapenda kugusia suala la diplomasia ya dijitali.
Ni wazi kuwa mapinduzi ya intaneti yameathiri utendaji kazi wa wizara mbalimbali za mambo ya nje duniani ikiwemo Tanzania kwenye masuala mbalimbali kama vile uchumi, siasa, jamii na usalama.
Diplomasia kama nyenzo mojawapo ya kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje haijaachwa kuathiriwa na mapinduzi haya katika teknolojia na hivyo kusababisha mabadiliko katika mikutano, biashara kimataifa, majadiliano, huduma za kifedha, muingiliano wa wajumbe, usuluhishi, usimamizi, utatuzi wa migogoro na usalama.

Kwa mantiki hiyo hakuna namna ambayo Tanzania itakwepa athari za teknolojia kama alivyowahi kubainisha Hayati Julius Kambarage Nyerere katika andiko lake Argue Don’t Shout (jenga hoja usibwate) la mwaka 1969.
Ni wazi kuwa teknolojia ni nguvu (power) ya kimya kimya au nguvu janja (soft power) kama alivyopata kubainisha Joseph Nye (1990: 176; 2004:5) kuwa ni nguvu janja na uwezo wa kujenga ajenda katika siasa za dunia kupitia ushawishi na kuwavutia wengine kupitia imani ya mtu au jamii husika, misingi na mawazo na si kupitia mabavu au nguvu za kijeshi.
Kwa maana nyingine ni uwezo wa kumfanya au kuwafanya wengine wafanye vile unavyotaka wewe pasina kutumia nguvu ya kijeshi au vikwazo.
Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kutumia teknolojia katika kutekeleza, kusimamia na kulinda maslahi ya taifa letu kupitia diplomasia ya dijitali.
Diplomasia ya dijitali ni dhana mpya ya diplomasia katika karne hii ya 21 ambayo imebadili mwenendo mzima wa utendaji kazi wa asili (traditional approach) wa Wizara za Mambo ya Nje na utekelezaji wa sera za nchi husika kama walivyobainisha Stanzel (2018) na Summa (2020).
Kwa tafsiri, diplomasia ya dijitali ni kuongezeka kwa utumiaji wa mitandao ya kijamii (social media) katika utekelezaji wa Sera za Mambo ya Nje za Nchi ili kufikia malengo yake ya maslahi ya taifa na kulinda taswira ya nchi na kusimamia mabadiliko kupitia vifaa vya kidijitali kama walivyobainisha Segev (2015) na Holmes (2015).
Ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia alieleza sababu za kuteua mabalozi wengi walio chini ya miaka 45, kwamba hawa wanaweza kwenda sambamba na teknolojia kuliko wazee na hivyo wasisubiri kupata taarifa kutoka (Capital’) wanapotakiwa kulinda taswira (image) ya nchi katika majukumu yao ya ubalozi yaliyobainishwa katika Ibara ya 3 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu uhusiano wa kidiplomasia.
Mheshimiwa Rais Samia ameona umuhimu wa diplomasia ya dijitali kutokana na ukweli kuwa jamii imekuwa na ufahamu mkubwa wa mambo yanayojiri duniani kwa haraka na kumekuwa na muingiliano mkubwa baina ya watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, Twitter na WhatsApp.
Leo hii Mtanzania anaweza kuona moja kwa moja kinachojiri Afrika Kusini au Tunisia kupitia simu yake kiganjani.
Mambo haya yanayojiri duniani yana athari kubwa katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje, utamaduni na usalama wa nchi na wakati fulani hutia presha kwenye maamuzi ya Serikali ama ya wananchi dhidi ya Serikali kama tulivyoona wakati ule wa vuguvugu la mapinduzi katika nchi za kiarabu, mwaka 2011 yaani Arab Spring. Rejea Kassim (2012) kujiridhisha.
Hivyo nirejee kusema kuwa teknolojia haikwepeki ni muhimu kwenda nayo kwani itasaidia kurahisisha utekelezaji wa sera kuliko njia ya kawaida kama alivyobainisha Jing (2017).
Lakini licha ya umuhimu huo, diplomasia ya dijitali haiwezi kwenda kama hakuna uwekezaji mkubwa kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kwa kifupi TEHAMA (ICT). Hili alilibainisha Adesina (2017). Kwa mantiki hiyo Tanzania inapaswa kuwekeza vema kwenye ICT ili kurahisisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na kulinda maslahi ya taifa.
Kwa bahati nzuri Serikali tayari ina Wizara ya TEHAMA, suala kubwa hapa ni kuwa na wataalamu wa kutosha katika eneo hilo, si tu wa TEHAMA bali wa diplomasia ya digitali pia.
NINI KIFANYIKE?
Kwa vile tayari Serikali ina Wizara ya TEHAMA na kuna sheria zinazoongoza habari, vyombo vya habari na mawasiliano, kunahitajika kuwepo na Sera ya Diplomasia ya Dijitali ambayo itapewa nguvu na sheria hizo.
Umuhimu wa kuwa na Sera ya Diplomasia ya Dijitali kutawezesha kuwa na kauli ya pamoja katika utekelezaji wa sera mbalimbali za Serikali kutokana na kurahisisha uratibu (coordination) katika dunia hii ya kidijitali, jambo alilowahi kuligusia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga.
Kwa mfano, kwa nchi kama Marekani anacho tweet Rais Joe Biden mtandaoni au kiongozi yeyote wa Serikali ya Marekani ndiyo msimamo (position) wa Marekani katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Marekani. Vivyo hivyo linafaa kuwa hivi kwetu.
Pili, nadhani sasa kuna haja kwa Serikali kuanzisha Ofisi/Afisi ya Diplomasia ya Dijitali ili kuhanikiza utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje kwa urahisi na kuwa na kauli moja juu ya nafasi ya Serikali katika jambo au mambo fulani yanayojiri.
Kwa mfano, nchi ya Uingereza ina Ofisi ya Diplomasia ya Dijitali na imeonesha kufanikisha sana utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Uingereza na tayari wana Balozi wa Dijitali ama Dijital Ambassador ambaye anashughulika na kulinda na kutetea maslahi ya Uingereza katika TEHAMA. Rejea Verrekia (2017) kubaini zaidi.
Kwa msingi huo, kuna haja kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa na Idara ya Diplomasia ya Dijitali kama ilivyo Idara ya Diplomasia ya Uchumi ili kufanikisha ufikiaji wa malengo ya nchi kisera.
Ni muhimu kuwa na kwa sababu kuu zifuatazo:
Mosi, uanzishwaji wa ubalozi wowote duniani hutegemea ridhaa ya pande mbili (mutual consent). Rejea ibara ya pili ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu uhusiano wa kidiplomasia.
Pili, kuna suala la jiografia na historia. Ukitazama Balozi za Tanzania nyingi kati ya 43 zilizopo sasa duniani zipo katika nchi ambazo ama tuna ukaribu nazo kimipaka (geographical proximity) ama tuna historia ama ya ukombozi ama ya kutawaliwa na Uingereza (Commonwealth).
Na kwa ujumla nyingi kati ya balozi zetu za moja kwa moja ambapo balozi huwepo (physically representation) zipo katika Jumuiya ya Madola.
Huenda ndiyo sababu hata Uingereza waliamua kubadili muundo wa Shirika la Misaada la Uingereza ama Idara (DFID) na Ofisi ya Mashauri ya Kigeni na Jumuiya ya Madola (FCO) kuwa Ofisi ya Masuala ya Kigeni, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) ili kulinda na kutetea maslahi yake katika nchi za Jumuiya ya Madola baada ya kujitoa Umoja wa Ulaya.
Jambo hili linaminya mawanda ya kupanua ushawishi kwenye nchi ambazo hatuna historia nazo ingawa ni muhimu kimkakati.
Nafahamu kuwa nchi ina nafasi ya kuwa na uwakilishi katika nchi zaidi ya moja (multiple accreditation) kama ilivyobainishwa kwenye ibara ya 5, ibara ndogo ya kwanza ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 (VCDR 1961), lakini bado ukweli unabaki kuwa diplomasia ya dijitali inaweza kuwa njia mbadala ya kufikia malengo ya Sera ya Mambo ya Nje na hasa tukizingatia uchache wa balozi zetu zilizopo duniani tukilinganisha na nchi kama Kenya ambayo ina balozi 163 duniani.
Kistratejia kuwa na balozi nyingi kama ilivyo Kenya kunatoa tafsiri ya uwezo wa nchi kufikia malengo yake ya Sera ya Mambo ya Nje hasa kupitia majadiliano (negotiations) ya moja kwa moja. Rejea ibara ya 3, kifungu ‘c’ negotiating with the government of the receiving State ya VCDR 1961.
Kutokana na uchache huo wa balozi zetu duniani kuna umuhimu wa kuwekeza kwenye TEHAMA ili kuipa nguvu diplomasia ya dijitali na kuwarahisishia mabalozi kazi ya kulinda, kutetea na kusimamia maslahi ya taifa.
Hivyo basi kwa kutumia diplomasia ya dijitali hata pale ambapo tumekosa uwakilishi wa moja kwa moja tunaweza kufikia malengo ya sera pasina kuhitaji uwakilishi wa kuwepo na jengo.
Kwa mfano, Marekani ilizindua Ubalozi wa Machoni (Virtual Embassy) mwezi Disemba, 2011 kule Tehran, Iran na inautumia ubalozi huo kufikia malengo yake ya Sera ya Mambo ya Nje pasina kuwa na ubalozi wa kuonekana (physical representation) kutokana na uhusiano wa nchi hizo kuvunjika mwaka 1979 kufuatia kupinduliwa kwa Shah aliyekuwa rafiki wa Marekani.
Kimsingi, lengo kuu la diplomasia ya dijitali ni kurahisisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje kwa kuipa nguvu diplomasia ya asili (Traditional Diplomacy) kupitia teknolojia ambayo ni nguvu isiyo na shuruti (soft power) ambayo humfanya mtu kufikia malengo au kumfanya mwingine atende jambo la huyo anaetaka jambo lake lifanywe pasina kutumia nguvu au vikwazo na hivyo mtu huyo kufanya jambo hilo bila kupenda kutokana na kuvutwa na nguvu ya ushawishi kutoka kwa mwenye jambo kama alivyobainisha Madu (2018) aliposema, ‘Digital Diplomacy allows countries to project their soft power beyond their borders.’
Hivyo diplomasia ya dijitali haiji kuua diplomasia ya asili bali inakuja kuipa nguvu katika kuwawezesha mabalozi na watekelezaji sera wengine wafanye kazi kwa urahisi.
Kimsingi diplomasia ya dijitali imekuja kuleta msawazo wa kibajeti baina ya nchi na nchi katika utekelezaji wa Sera za Mambo ya Nje, kubwa na la muhimu ni kuwekeza katika TEHAMA na kuwa na wataalamu wa kutosha, wenye weledi wa TEHAMA na diplomasia ya dijitali ili kusaidia kuitafsiri Sera ya Mambo ya Nje na sera nyingine kwa lugha nyepesi ambayo mwananchi wa kawaida ataweza kuielewa na kushiriki katika utekelezaji wake.