Saturday, March 15, 2025
spot_img

CHOZI LA NDOA LAIBUA TUHUMA MPYA

Michael Laiser na Pamela Kayira

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

MICHAEL Laiser anayelia kusalitiwa, kuteswa na kutelekezewa watoto na mkewe Pamela Kayira ameibua tuhuma mpya udanganyifu na kughushi uraia dhidi ya mtu anayedai kuwa ndiye anayeivuruga ndoa yake.

Laiser amemtaja mtu huyo kuwa ni Patricia Kayira, dada wa mke wake Pamela kuwa siyo raia wa Tanzania na mwenendo wa maisha yake amekuwa akiutilia shaka tangu alipomfahamu.

Tuhuma hizo ambazo amekuwa akizitoa kwa zaidi ya wiki mbili sasa, wiki iliyopita alizirejea tena kwa msisitizo katika mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog ambayo inaripoti habari za mgogoro wa ndoa yake kwa kueleza kuwa Patricia ameanza kuwatisha baadhi ya watu anaohisi kuwa wanatoa taarifa zake za siri kwa waandishi wa habari.

Laiser alisema, Patricia ni dada mkubwa wa mke wake Pamela ambao baba yao, raia wa Burundi aliyeingia nchini kinyume cha taratibu na kuoa mwanamke mtanzania na kwamba wawili hao walijawa kupata watoto kadhaa, wakiwemo Patricia na Pamela.

Patricia Kayira

 

Kwamba Patricia na Pamela ambao waliishi na kusoma hapa nchini walipaswa kufuata sheria za uhamiaji baada ya kufikisha miaka 18 kwa kuthibitisha uraia wao na kuukana uraia wa Burundi, jambo ambalo hawajapata kulitekeleza na aliongeza kuwa Patricia anayo mambo ya siri yanayopaswa kuchunguzwa na vyombo vya dola.

“Huyu mwanamke, Patricia ana mambo yake ya siri ambayo anayafanikisha kwa kumtumia huyu mke wangu. Mimi nimewafahamu hawa miaka zaidi ya 20, na nimejifunza mengi sana kwao na hivi karibuni ndiyo nimegundua kuwa mbali na shughuli zake nyingine ambazo anazijua mwenyewe lakini siyo raia, ila ni mjanja sana. 

“Hawa baba yao ambaye ni marahemu, mzee Bartholomew Samson Kayira, aliingia hapa nchini kama mhamiaji haramu, akaoa mwanamke mtanzania ndiyo wakazaliwa kwanza huyo Patricia na ndugu zake wengine, Pamela mke wangu ni wa mwisho, hivyo katika familia yao wanawake wapo wawili tu.

“Mimi nilipokutana naye nilianza kumsomesha huyu Pamela, tukawa wachumba, kila kitu chake alikuwa anaagizwa na kusimamiwa na Patricia, nikawa namuuliza wazazi wapo wapi naye alisema walishafariki mlezi wake ni dada yake Patricia. Hivyo hata kwenye ndoa yetu kulikuwa na ndugu wachache wa upande wa mama yao lakini kwa baba yao hakuwepo hata mmoja. Kulikuwa na mama mmoja hivi sijui Patricia alimtoa wapi ndiye aliombwa ajifanye kama mama yake mzazi.

“Baada ya ndoa sasa. Kwanza Patricia anafanya kazi (anataja jina taasisi moja isiyokuwa ya kiserikali, lakini tunahifadhi jina kwa sasa) nyendo zake ni siri sana, haruhusu ndugu yoyote wa upande wa baba yao amtembelee kutoka Burundi na mambo yake kweli mimi siwezi kusema sana labda vyombo vya uchunguzi vikifanya kazi vitasema.

“Ninaloweza kusema ni kwamba siyo raia. Ni kweli alizaliwa hapa nchini lakini hajawahi kuthibitisha uraia wake na amemkataza hata mdogo wake, mke wangu kuukana uraia wa Burundi na kuthibitisha uraia wa Tanzania. Anakaribia kustaafu kazi hapo anapofanyia na nasikia sikia kwa mke wangu kuwa muda wao wa kukaa nchini umekaribia kuisha na kazi yao wameifanya vizuri hivyo wanajiandaa kurudi kwao.

“Hapo awali kabla uhusiano wetu haujawa mbaya, nilikuwa namuuliza Pamela usiku anaenda wapi harudi nyumbani wakati ana watoto na wakati mwingine anapotea kabisa miezi mingi hajulikani alipo anasema kuna kazi muhimu za dada yake anamsaidia lakini hizo kazi hazisemi. Ni siri yao wenyewe. Mpaka alipomtafutia huyo mwanaume ili ijulikane kuwa na mwanamume mwingine huwa anakuwa huko kuficha siri ya wanachokifanya. Alimtafutia kwa sababu maalumu lakini mke wangu ndiyo kakolea sasa anasambaratisha ndoa yetu,” alisema Laiser.

Tanzani PANORAMA Blog ilimtafuta Patricia kupitia simu yake ya kiganjani kumuuliza kuhusu madai hayo naye katika majibu yake alisema yeye ni raia halali wa Tanzania na amezaliwa na wazazi wote wawili, baba na mama watanzania.

Patricia alisema, Laiser ameamua kumchafua baada ya kuona anamsaidia mkewe ambaye ameshindwa kumtunza hivyo huwa anakwenda kula na kulala kwake kukwepa kero za mumewe na aliomba kuonana ana kwa ana na mwandishi kwa mahojiano kwa sharti kuwa awe na mwanasheria wake na askari polisi.

Patricia Kayira

 

Tanzania PANORAMA Blog ilimkaribisha Patricia, mwanasheria wake na askari atakaohitaji kuwa nao na ilimpa uwanja mpana zaidi wa kuchagua mahali anapotaka mahojiano yamefanyike ikiwemo kituo chochote cha polisi, mahakamani au ofisi ya uwakili atakayochagua naye aliomba muda wa kuwasiliana na mwanasheria wake kabla ya kutoa jibu.

Katika hatua ya kushangaza, Patricia hakurejea kama alivyoahidi na alipopigiwa simu yake iliita bila kupokelewa. Alipopigiwa tena na tena alikata simu na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi katika simu yake ya kiganjani hakujibu.

Kwa mujibu wa sheria, mtoto anayezaliwa nchini baba yake akiwa raia wa kigeni anakuwa na uraia pacha mpaka anapofikisha umri wa miaka 18 ambapo anatakiwa kuchagua uraia wa nchi moja na iwapo anataka kuwa raia wa Tanzania anatakiwa kuukana uraia mwingine kinyume cha hapo uraia wake wa Tanzania unakuwa umekoma.

Laiser alipoulizwa ni kwanini hakutoa taarifa mapema kwa vyombo vya dola kuhusu utata wa uraia wa Patricia na Pamela ambaye ni mke wake pamoja na mashaka aliyonayo kuhusu nyendo za Patricia alisema; “Ni jambo ambalo nimeligundua hivi karibuni tayari tukiwa na watoto na ukumbuke huyo Pamela ni mke wangu.

“Na ujue Patricia siyo mwepesi kama unavyomfikiria, kwanza ofisi anayofanyia kazi ina nguvu kubwa sana na yeye ni ofisa wa juu hapo, kwenye hiyo ofisi nendeni wenyewe mtaona lakini mjue analindwa, ana mtandao, ana nguvu. Hivyo kumwendea hovyo hovyo kuna ghamara zake.

“Lakini kama anasema yeye ni raia hebu muulizeni baba yake kazaliwa wapi na ni kabila gani? Ndugu wa baba yake wanaitwa nani na wapo wapi?

“Alishawahi kumuona ndugu yoyote wa baba yake (baba mdogo, baba mkubwa au shangazi? Kama ndiyo wanaishi wapi? Kama wamefariki makaburi yao yapo wapi? Kwenye harusi ya Pamela na Michael kuna ndugu yoyote wa baba aliyehudhiria? Kama ndiyo ni akina nani na kama hapana ni kwa nini?

“Je aliwashawahi kwenda mahali, kijiji au kata ambapo baba yake alizaliwa? Babu na bibi kwa upande wa baba wapo hai? Kama wamefariki anaweza kwenda kuonyesha makaburi yao, tuanze na hayo?” alisema Laiser.

Wiki iliyopita Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa mgogoro unaosababishwa na usaliti wa mapenzi ndani ya ndoa ya wanandoa Michael Laiser na Pamela Kayira umesababisha watoto wao kukosa haki ya malezi bora.

Michael, mume wa Pamela ndiye aliyefichua kuwepo kwa hali ya hofu na wasiwasi ndani yanfamilia yake katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine alimtuhumu mkewe kuwa chanzo cha kuwepo kwa hali hiyo kutokana na vitendo vyake vya kusaliti penzi lao na kuwatelekeza watoto wao.

Katika mahojiano hayo, Michael alimtuhumu Pamela kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanamume mwingine, kuipa kisogo familia yake, (mumewe Michael na watoto wao watatu), kuwa na kiburi na jeuri, kuondoka nyumbani asubuhi kwenda kazini na kurudi asubuhi ya siku inayofuata akiwa hajulikana alikolala huku akijua kuwa uraia wake pamoja na wa dada yake ni wa mashaka pamoja  na kuhama nyumbani kwake kwa muda wa miezi sita kwenda kuishi mahali kusikojulikana.

Michael alisema amemgundua mkware mwenye uhusiano wa kimapenzi na mkewe na anamuomba amuonee huruma kwa sababu kitendo anachokifanya kina athari mbaya katika maisha ya watoto wake na kinaiharibu familia yake. Pia alimuomba mwajiri wa mkewe asaidie kuokoa ndoa yake na watoto kupata mapenzi na malezi ya mama yao.

Kwa upande wake Pamela alizipuuza tuhuma hizo. Katika mahojiano aliyofanya na Tanzania PANORAMA Blog, Pamela alikataa kutoa ushirikiano na aliikana ofisi anayofanyia kazi.

Dk/ Germana Leyna

 

Wakati Pamela akipuuza tuhuma na kilio cha mumewe, bosi wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dk. Germana Henry Leyna naye alikataa kuthibitisha kama Pamela ni mfanyakazi wa taasisi anayoiongoza au lah na alijiweka mbali na ombi la Michael la kumkalisha kitako Pamela kumsihi kuijali familia yake na hasa kulea watoto wake.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya