Tuesday, June 17, 2025
spot_img

MKUTANO BARAZA LA VYAMA VYA SIASA KUTATHMINI UTEKELEZAJI, KUONGEZA UWAZI, KUIMARISHA AMANI – MHAGAMA

RIPOTA PANORAMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema mkutano wa siku tatu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoanza leo Jijini Dar es Salaam una faida kubwa tatu kwa wadau wa siasa, demokrasia na nchi kwa ujumla.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Waziri Mhagama alisema mkutano huo utakaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), umeandaliwa mahususi kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mhagama alizitaja faida za mkutano huo kuwa ni kutoa fursa kwa wadau wa demokrasia nchini kutathmini mapendekezo ya Kikosi Kazi jinsi  yalivyotekelezwa.

Alisema tathmini hiyo itasaidia kuona mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza katika kukuza demokrasia ya vyama vingi nchini.

Aliitaja faida ya pili ya mkutano huo kuwa, utachangia kuongeza uwazi katika mchakato wa kisiasa na kuboresha uhusiano kati ya vyama vya siasa na Serikali na kwamba hilo litapunguza migogoro na kuleta utulivu wa kisiasa nchini.

Alisema, faida ya tatu imebebwa na kauli ya mbiu ya mkutano wenyewe ambayo ni ‘Imarisha Demokrasia, Tunza Amani.’

“Kauli mbiu hii inaonyesha dhamira ya kudumisha amani katika mazingira ya kisiasa. Mkutano huu unaweza kusaidia kusuluhisha migogoro ya kisiasa na kuzuia vurugu, hivyo kuweka msingi thabiti wa amani nchini.

Akizungumzia madhumuni ya mkutano huo, Waziri Mhagama alisema unalenga kuchunguza mapendekezo ya Kikosi Kazi na kubainisha maeneo ambayo yamefanikiwa na yale ambayo yanahitaji kurekebishwa ili kuboresha demokrasia ya vyama vingi.

Alisisitiza kuwa madhumuni ni kuhakikisha kuwa maboresho yanafanyika ili kuendeleza demokrasia.

Alisema mkutano huo unatoa jukwaa la kuwasilisha maoni na masuala ya wadau wa demokrasia, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa na jumuiya zao na kwamba hilo litaongeza ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kisiasa na maendeleo ya nchi.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, Ikulu, Dar es Salaam muda mfupi baada ya kutoka gerezani. (Picha na maktaba)

Waziri Mhagama alisema dhumuni jingine ni kujenga uhusiano mzuri kati ya Serikali, vyama vya siasa na wadau wengine katika jitihada za kuimarisha demokrasia na kudumisha amani nchini.

“Uhusiano mzuri unaweza kusaidia kuleta maridhiano na ushirikiano katika kufanikisha malengo ya kisiasa na maendeleo ya nchi. Mkutano huu unalenga kuendeleza demokrasia nchini Tanzania kwa kuchambua utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi, kuimarisha uwazi, kudumisha amani, na kuwapa sauti wadau wa demokrasia,” alisema Waziri Mhagama.

Akizungumzia jinsi Rais Samia anavyotumia kanuni za demokrasia, maridhiano na ustahimilivu katika sera na maamuzi yake kwa lengo na kukuza amani na maendeleo hapa nchini na Afrika kwa ujumla, Waziri Mhagama alisema ni muhimu kuwa na uelewa wa kina wa jinsi Rais Samia anavyotumia kanuni za demokrasia, maridhiano na ustahimilivu katika sera na maamuzi yake.

“Ni muhimu kuwa na uelewa wa kina wa jinsi Rais Samia Suluhu Hassan anavyotumia kanuni za demokrasia, maridhiano na ustahimilivu katika sera na maamuzi yake. Ni muhimu kuchambua jinsi anavyoendesha uongozi wake kwa lengo la kukuza amani na maendeleo katika Tanzania na Afrika kwa ujumla. Hapa kuna baadhi ya mifano ya jinsi anavyoweza kutumia kanuni hizi.

“Kwanza demokrasia. Rais Samia ameendeleza mfumo wa uchaguzi huru na wa haki nchini. Tangu alipoingia madarakani amehakikisha vyama vya upinzani vinafanya kazi na vina nafasi ya kushiriki katika siasa za nchi.

“Pili kuna ishara za kuendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na kujaribu kuboresha mazingira ya waandishi wa habari nchini,” alisema Waziri Mhagama.

Katika hilo, Waziri Mhagama aliendelea kueleza kuwa Rais Samia anasikiliza maoni na matatizo ya wananchi na amefanya mikutano mingi ya hadhara ili kujenga mawasiliano na kuwasiliana moja kwa moja na raia.

Alisema tangu alipoingia madarakani, Rais Samia amejitahidi kujenga umoja na kuleta maridhiano nchini na kwa kauli thabiti amekuwa akisisitiza umuhimu wa kusitisha migawanyiko ya kisiasa na kikabila.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (Picha na maktaba)

“Kwa makusudi, Rais Samia anashirikisha vyama vyote vya siasa katika mchakato wa kuleta maendeleo ya Taifa na kujenga mazingira ya kisiasa yenye utulivu na ameonyesha nia ya dhati ya kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria ambayo ni msingi wa ustahimilivu na utulivu wa kisiasa.

“Rais Samia amekuwa akitafuta suluhisho la amani katika migogoro ya ndani na katika eneo la Afrika kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuwa mpatanishi katika mizozo ya kikanda.

“Na kauli yake dhidi ya ufisadi ni kali. Rais Samia ametoa kauli kali dhidi ya ufisadi na amechukua hatua za kupambana na ufisadi ndani ya Serikali. Hii inaongeza ustahimilivu na uaminifu katika Serikali yake,” alisema Waziri Mhagama.

Alisema ni muhumu kuzingatia kuwa tathmini ya uongozi wa Rais Samia inaweza kutofautiana na maoni ya watu na wachambuzi wengine na kwamba bado kuna changamoto kadhaa za kisiasa na kiuchumi zinazohitaji kutatuliwa.

Mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa utakaowashirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi na kujadili hali ya kisiasa nchini, unafunguliwa leo na Rais Samia na utafungwa Jumatano, Septemba 13, 2023 na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya