*Aonya wizara isigeuke mtatuzi wa migogoro
TERESIA MHAGAMA
Dodoma
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kupanga, kupima na kimilikisha ardhi kwa ufanisi.
Amesema utekelezaji wa majukumu ya msingi kwa ufanisi kutaondoa migogoro ya ardhi inayotokea nchini na kuifanya wizara kuishughulikia mara kwa mara.
Akizungumza jana wakati wa hafla ya kuzindua Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Taarifa za Kijiografia iliyofanyika Jijini Dodoma, alisema kazi za msingi za wizara hiyo ni tatu ambazo ni kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.
Dk. Biteko ambaye alimuwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye halfa hiyo alisema wizara inapaswa kujipima na kujitathimini iwapo inatekeleza kikamilifu majukumu yake.
“Kazi za wizara hii ni tatu, ambazo ni kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Sasa tujipime na tujitathmini kama katika sekta yetu ya ardhi kazi hizi tunazifanya kwa ukamilifu wake.
“Lipo wimbi la kuweka tension ya wizara kutoka kwenye sheria yake au Ilani ya uchaguzi na kugeuka kuwa wizara ya utatuzi wa migogoro ya ardhi. Kuanzia sasa tuwafanye Watanzania wazungumze mipango miji, maendeleo ya makazi na matumizi bora ya ardhi.” alisisitiza Dk. Biteko
Naibu Waziri Mkuu huyo aliitaka wizara hiyo kushirikiana na halmashauri zote nchini ili kazi zifanyike kwa ufanano; kuondoa urasimu na migogoro ya ardhi.
Alieleza matumaini yake kwa wizara hiyo kumaliza changamoto zilizopo na kutekeleza kwa ufanisi upangaji miji ili kuimarisha makazi ya watu na kujenga Tanzania iliyo bora zaidi.
“Wizara hii ni moyo wa shughuli za uchumi hapa nchini kwani watu wanaofanya shughuli za ujenzi, kilimo, wanaojenga miradi mbalimbali ikiwemo ya gesi asilia, wanategemea Sekta ya Ardhi. Pamoja na kazi kubwa iliyofanyika ya kuimarisha sekta hii bado kuna kazi kubwa mbele ya kujiimarisha,” alisema Dk. Biteko
Akizungumza kuhusu kituo alichokizindua, alisema ni muendelezo wa hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchochea matumizi ya teknolojia kuleta maendeleo endelevu na ubunifu hapa nchini.
Alisema kituo hicho ni muhimu kwani kitaboresha shughuli za upimaji ardhi, uandaaji wa ramani za msingi, ujenzi wa miundombinu, kupanga matumizi bora ya ardhi pamoja na masuala mengine yanayohusiana na Sekta ya Ardhi.
Dk. Biteko alitoa wito kwa wizara na taasisi zake kupeleka watumishi kwenye kituo hicho kujifunza ukusanyaji, uchakataji na utumiaji wa taarifa za kijiografia wanapotekeleza majukumu ya taasisi zao.
Aidha, alikipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kutoa eneo na jengo kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho na pia aliishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa kugharamia uanzishaji wake.
Aliwaasa watakaohitimu kwenye kituo hicho kwenda kufundisha watumishi wengine na kuwa chachu ya mabadiliko ya kiutendaji katika Sekta ya Ardhi na kuongeza matumizi ya taarifa za kijiografia nchini.