![]() |
Jengo la ghorofa linalotumiwa ma wafanyabiashara Akif Kara na Ugur Gurses kulangua umeme |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
IDADI ya wafanyabiashara wanaocheza mchezo mchafu wa kununua uneme wa TANESCO kwa bei ndogo na kuuuza kwa bei ya ulanguzi kwa watu waliopanga katika majengo yao imezidi kuongezeka.
Mfanyabiashara Akif Kara wa Kampuni ya Mar Kim Chemicals ya jijini Dar es Salaam ambaye pia ni mbia katika umiliki wa jengo la ghorofa lililopo Mtaa wa Livingstone Kariakoo, naye ametajwa kujihusisha na mchezo huo mchafu.
Imeelezwa kuwa Akif amekuwa akilangua umeme wa Tanesco kwa zaidi ya miaka mitano sasa na pia amefanya biashara hiyo bila kuwa na leseni ya EWURA kwa kipindi hicho.
Alipoulizwa Akif kuhusu tuhuma hizo alisema hawezi kuziongelea na kuelekeza atafitwe mwanasheria wake ambaye pia ni msemaji wake.
Muda mfupi baada ya Akif kuulizwa hilo, mtu aliyejitambulisha kwa jina la Albert Kimaro, mwanasheria wa Akif alipiga simu na kueleza kuwa yeye ndiye mzungumzaji wa Akif hivyo atafutwe ana kwa ana kwa ajili ya kutoa ufafanuzi.
Kimaro alipokutana na Tanzania PANORAMA Blog alisema ni kweli Akif hapo awali alikuwa akijihusisha na mchezo huo mchafu lakini wiki iliyopita baada Tanzania PANORAMA kuripoti kuwepo kwa tuhuma za aina hiyo, alimpa maelekezo ya kushusha bei kwa kiwango kilichowekwa na EWURA.
Awali Tanzania PANORAMA Blog iliripoti malalamiko yaliyotolewa na Haykal Hassan dhidi ya vitendo vya ulanguzi umeme vinavyofanywa na Ugur Gurses.
Hassan alisema yeye amenunua moja ya ghorofa katika jengo hilo lakini Gurses amekataa kumruhusu kuweka mita yake kutoka TANESCO na badala yake anamuuzia umeme kwa shilingi kati ya 650 na 500 kwa uniti moja.
“Mimi nimenunua ghorofa hapa, lakini huyu jamaa mpaka leo anatulangua umeme kinyume kabisa na maelekezo ya Serikali. Tangu niliponunua mpaka mwaka 2020 alikuwa anatuuzia sh 650 kwa uniti moja tukalalamika sana mpaka kwenye vyombo vya Serikali ndiyo akashusha kidogo akawa anatuuzia sh. 500.
“Kikawaida mimi baada ya kununua ghorofa yangu nilipaswa kuwa na mita yangu na ningekuwa nanunua umeme wa TANESCO lakini hapa kuna hizi mita za Bahdea wanatulangua kweli.
“Wameishakuja maafisa wa Serikali hapa na kuelekeza bei ishushwe lakini Gurses aliwakatalia akasema hashushi na kweli hakushusha na hajafanywa lolote,” alisema Hassan.
Alipoulizwa meneja wa jengo hilo, Gibson Gabriel kuhusu ulanguzi huo wa umeme alisema ni kweli kuna tatizo kwenye bei lakini mamlaka za serikali kukosa nguvu ya kusimamia sheria ndiyo kunaumiza wananchi na kuwapa kiburi baadhi ya watu wenye fedha.
“Ni kweli hapa kuna tatizo, ni la siku nyingi.
Hili jengo linamilikiwa na watu wawili. Kuna huyo Gurses na kuna Akif wa Mar-Kim Chemicals Co. LTD. Hizo ghorofa za juu zote wanaziuza na kuna wapangaji.
“Tanesco wana mita yao moja hapa ambayo ndiyo kubwa na wamiliki wamenunua mita ndogo ndogo kwa Kampuni ya Bahdea na kusambaza kila ghorofa. Hivyo wao huwa wanailipa na Tanesco na wanawauzia wakazi wengine wa humu.
“Tatizo ni kwamba bei wanayowauzia ni kubwa sana siyo iliyopangwa kisheria. Wamelalamika mpaka kwenye mamlaka za Serikali na barua zao zipo, hao maofisa wakaja hapa yule Mar- Kim Chemicals Co. LTD akakubali kushusha hadi sh 350 kwa unit ila huyu Gurses aligoma. Wakaondoka naona hawakuwa na uwezo wa kumfanya chochote ila wanaoumia ni wapangaji maana bei ni kubwa mno,” alisema Gabriel.
Alipoulizwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha EWURA, Titus Kaguo kuhusu kadhia hiyo alisema EWURA iliruhusu watu wenye majumba makubwa ambapo wamepanga wengi kutumia mita ndogo.
“EWURA iliruhusu kutumia Sub-meters, kwa maana kwamba mita ya Tanesco inawekwa pale unapoingilia umeme ambao kimsingi mara nyingi unakuwa umenunuliwa in bulk(kwa ujumla) then ili mpangaji kulipa kadri anavyotumia anawekea sub mita( mita ndogo) lakini gharama ya umeme haitakiwi kuzidi shilingi 292/- kwa UNIT Kwa T1 ambao unatumika majumbani.
“Therefore, Bahdea anatakiwa kutoza sh 292 kwa unit ambayo ilipitishwa na EWURA kwa matumizi ya majumbani.
Kama sivyo; watu wanatakiwa kuleta malalamiko katika ofisi zetu za Kanda ya Mashariki Kijitonyama PSSSF Ghorofa ya saba,” alisema Kaguo.
Mar Kim Chemicals inakuwa kampuni ya pili kubainika kukiuka sheria za nchi huku UWERA ikiwa imeishaeleza kuwa Gurses shauri lake lineishafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Uchunguzi zaidi dhidi ya vitendo hivi vya ulanguzi na jinsi kampuni hizi zilivyojinufaisha kwa kukiuka sheria unaendele.