RIPOTA WA WAZIRI MKUU
Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeanza kufanyia kazi taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) baada ya kuwasilishwa bungeni Aprili 6, mwaka huu.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo bungeni Jijini Dodoma, Aprili 13, 2023 wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakijadili mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
āTarehe 6 Aprili, 2023 taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliwasilishwa hapa bungeni ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kikatiba linaloielekeza Serikali kuwasilisha bungeni taarifa hiyo ndani ya siku saba za kazi kuanzia siku ya kikao cha kwanza cha Bunge tangu ilipowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais.
āNitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa bungeni, tayari Serikai kwa upande wake imeanza kuifanyia kazi mara moja,ā alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Alisema anatambua hisia za wabunge pamoja na wananchi kuhusu ubadhirifu wa mali na fedha za umma uliobainishwa kwenye taarifa hiyo.
āSote tulishuhudia namna Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoonyesha kutoridhishwa na ubadhirifu uliobainishwa kwenye taarifa hiyo,ā alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa alilieleza Bunge kuwa miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha maafisa masuuli wanaandaa majibu ya hoja kama inavyoelekezwa na sheria na kanuni za ukaguzi wa umma.
āNitumie fursa hii kuwakumbusha maafisa masuuli wote wezingatie maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha wanap;itia kwa kina taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kujibu na kuchukua hatuaa za haraka juu ya hoja zote zilizoibuliwa kwenye maeneo yao,ā alisisitiza.
Waziri Mku Majaliwa alisema pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali, taarifa ya kina kwenye maeneo yaliyobainishwa katika ripoti ya CAG itawasilishwa bungeni kwa kuzingatia kanuni husika.
āNalihakikishia Bunge na wananchi kuwa kwa kuzingatia msimamo wa Mheshimiwa Rais, Serikali ya Awamu ya Sita haitafumbia macho matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kuwa hatua zinazochukuliwa zitakuwa endelevu,ā alisema.
Bunge liliidhinisha bajeti ya Shilingi 339,361,007,000 ambapo Shilingi 173,733,110,000 ni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake na Shilingi 165,627,897,000 ni kwa ajili ya mfuko wa Bunge.
Akiwasilisha makadirio na matumizi ya ofisi yake Aprili 5, mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa aliliomba Bunge liidhinishe Shilingi 173,733,110,000, kati ya fedha hizo, Shilingi 121,364,753,320 ni kwa ajili ya matumuzi ya kawaida na Shilingi 52,368,356,680 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Vile vile aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya Shilingi 165,627,897,000 kwa ajili ya mfuko wa Bunge, Shilingi 160,458,877,000 ni kwa matumizi ya kawaida na Shilingi 5,169,020,000 kwa ajili ya matumuzi ya maendeleo.