Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa |
RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameunda kamati maalum ya watu tisa ambayo imepewa jukumu la kuchunguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi, Tanga.
“Kamati hiyo inapaswa kuanza kazi yake kesho na inatakiwa iwe imekamilisha ripoti yake ndani ya siku 14,” amesema Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa, Ijumaa, Februari 4, 2022 mjini Magu, Mwanza akiwa njiani kuelekea Musoma, mkoani Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumzia mauaji hayo, Rais Samia alisema anatambua Jeshi la Polisi limeunda kamati ya uchunguzi lakini aliagiza iundwe kamati huru ili ikafanye uchunguzi wa mauaji ya Mtwara yaliyodaiwa kufanywa na askari polisi.
Polisi wanatuhumiwa kufanya mauaji ya raia mkoani Mtwara Januari 5, 2022 na mauaji mengine wanadaiwa kufanya huko Kilindi mkoani Tanga Januari 30, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, kamati hiyo ina maafisa wenye dhamana kutoka mamlaka tofauti za Serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, TAKUKURU, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro |
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kuwasimamisha kazi maafisa wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara na Kilindi mkoani Tanga kupisha uchunguzi wakati kamati aliyoiunda ikifanya uchunguzi.
“Viongozi hawa wanapaswa wakae pembeni, watahojiwa na hii timu wakiwa nje ya ofisi,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuwataja maafisa hao kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara (RPC), Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mtwara (RCO) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara ambako mfanyabiashara Mussa Hamisi Hamisi anadaiwa kupoteza maisha.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kilindi na afisa upelelezi wa wilaya hiyo nao kukaa pembeni kupisha uchunguzi.