ABBAS MWALIMU
0719 25 84 84
MJADALA mkubwa kwa sasa ni ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere inayojadiliwa bungeni, Dodoma.
Ripoti ya CAG inaonesha kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na yasiyozingatia bajeti katika wizara, taasisi, wakala na idara kadhaa za Serikali hali ambayo imezua mijadala na maswali mengi kutoka kwa wananchi.
Aidha, ni wazi kuwa ripoti hii ya CAG imeshtua watu wengi sana na kuzua maswali kadha wa kadha. Kadhalika ripoti ya CAG inaonesha wazi kuwa kuna changamoto kubwa ya uadilifu na uwajibikaji nchini.
Vilevile, ripoti hii ya CAG inadhihirisha haja ya kufanya mageuzi (reform) ya kitaasisi ili kukidhi mahitaji ya wakati.
Sambamba na hilo, ipo haja ya kufanya mageuzi ya mfumo wa ukaguzi na uthibiti wa matumizi ya fedha za umma ili kuongeza uwajibikaji kwa watumishi.
Hoja hii ya mageuzi ni muhimu sana wakati huu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekuja na R nne ama 4R kwa lugha ya Kingereza.
Kimsingi, tatizo la CAG ni moja na ni kubwa. Tatizo hili ni la maamuzi. CAG hana maamuzi yenye uwezo wa kuathiri moja kwa moja (Sanctioning/enforcing decisions).
CAG amekuwa akishauri tu jambo linalotoa mwanya kwa baadhi ya watumishi wasio waadilifu kuendelea kutumia ofisi za Serikali kwa manufaa yao binafsi.
Halikadhalika, licha ya chama kinachoisimamia Serikali kuonesha nia yake ya kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na ubadhilifu wa fedha za umma wanachukuliwa hatua, lakini bado msimamo huo wa chama hauondoi haja ya kuwa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi yenye meno.
NINI KIFANYIKE?
Wakati huu ambapo ripoti ya CAG inajadiliwa bungeni kuna umuhimu wa Bunge kutoa msimamo wake.
Msimamo huu unaweza kuja katika sura ya azimio la kuitaka Serikali kuchukua hatua za kisheria kufanyia kazi mapendekezo na ushauri wa CAG.
Kwa kufanya hivi Bunge litakuwa limetekeleza wajibu wake kwa mujibu wa ibara ya 63, ibara ndogo ya pili na ya tatu za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake.
Aidha, kuna haja sasa kwa Bunge kuja na hoja ya kutaka Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi ifanyiwe mageuzi ya kitaasisi ili kuakisi dhana ya reforms anayoisimamia Rais Samia Suluhu Hassan.
Wabunge wana haki na wajibu wa kufanya hivi kwa kuzingatia kifungu cha 58 mpaka cha 64 cha kanuni za kudumu za Bunge, toleo la mwezi Juni, 2020. Pia, Bunge lina mamlaka ya kufanya hivyo kwa mujibu wa ibara ya 98 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo basi, kuna haja ya kuifanyia mageuzi Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi – National Audit Office (NAO) kuwa Mamlaka ya Taifa ya Ukaguzi – National Audit Authority (NAA).
KWA NINI NAA?
Kwa sababu NAO ikifanyiwa mageuzi kuwa mamlaka kamili (Authority) kwa maana ya NAA itakuwa na uwezo wa kimaamuzi (ability to enforce sanctions).
Kwa muktadha huo, NAA itakuwa na uwezo wa kuwawajibisha wabadhilifu wa fedha za umma moja kwa moja kwa mujibu sheria itakayowekwa.
Hivyo NAA itakuwa na uwezo wa kushitaki au kufungua mashitaka dhidi ya wabadhilifu badala ya kuishia kushauri ‘Mamlaka’ tu kama ilivyo sasa.
Kwa mantiki hiyo, ili Serikali iweze kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma hakuna budi kuifanyia mageuzi Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi kwa kuipa uwezo wa kuathiri (ability to sanction) kwa sababu hicho ndicho kinachokosekana.
Hili liligusiwa pia na Razanno na Gruzd (2015) pia walipoeleza kwa lugha ya Kingereza kwamba, “…the lack of tough sanctions may mean that the political reputational incentive is not significant enough to warrant change.”
Ipo baadhi ya mifano ya taasisi zilizoonesha mafanikio makubwa baada ya kufanyiwa mageuzi ya kitaasisi. Kwa mfano, mafanikio ya TAKUKURU yalianza kuonekana pindi ilipoanza kujitegemea kwa kufanyiwa mageuzi ya kitaasisi.
Vivyo hivyo, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa baada ya kufanyiwa mageuzi ya kitaasisi. Bila shaka NAA nayo itafanikiwa sana endapo itafanyiwa mageuzi ya kitaasisi.
Aidha, ipo haja pia ya kufanya mageuzi ya mfumo wa ukaguzi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma. Ripoti ya CAG inaonesha kuwa madudu mengi yameibuliwa baada ya miradi kwisha na kukaguliwa.
Ni muhimu sasa kwa CAG kuhama kutoka kwenye ukaguzi wa baada na kujikita kwenye ukaguzi wa muda halisi-real time auditing ili kwenda sambamba na miradi na matumizi mbalimbali yanayofanyika.
Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).