RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 3,826 katika kuadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamadi Masauni, Rais Samia kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba ya Tanzania, ametoa msamaha huo huku akielekeza kuzingatia mambo 18.
![]() |
Rais Samia Suluhu Hassan |
Taarifa ya Waziri Masauni inayataka mambo hayo kuwa ni wafungwa wote wapunguziwe robo ya vifungo vyao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha sheria ya Magereza, sura ya 58.
Kwamba wafungwa hao sharti wawe wametumikia robo ya vifungo vyao na wawe wameingia gerezani kabla ya Februari 26, 2022 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika sharti la pili (i hadi ii).
Sharti la pili linawahusu wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu ambao wametumikia robo ya vifungo vyao na wafungwa wazee kuanzia umri wa miaka 70 ambao wametumikia robo ya vifungo vyao.
Pia wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa na watoto wanaonyonya, wasionyonya na wajawazito ambao wametukimia robo ya vifungo vyao na wafungwa wenye ulemevu wa mwili na akili ambao wametumikia robo ya vifungo vyao. Wote hao watahitaji uthibitisho wa jopo la waganga ambalo litakuwa chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Masharti mengine ni wafungwa waliotumikia adhabu ya kuwekwa kuzuizini waliokaa kuanzia miaka 10 na kuendelea, wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 30 na kuendelea na wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani ambao wamekaa gerezani kuanza miaka 20 na kuendelea.
Pia wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya kujaribu kuua ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 na kuendelea, wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya kujaribu kujiua waliokaa gerezani kuanzia miaka 15 na kuendelea na wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya uhujumu uchumi ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 20.
Masharti hayo yanawagusa pia wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya matumuzi mabaya ya madaraka ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka mitano, wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya utakatishaji wa fedha waliokaa gerezani kuanzia miaka 20, wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya rushwa waliokaa gerezani kuanzia miaka 10 na wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya wizi au ubadhirifu wa fedha na mali za umma waliokaa gerezani kuanzia miaka 15.
Aidha, taarifa ya Waziri Masauni inaeleza kuwa msamaha huo hauwahusu waliofungwa kwa makosa ya madeni na wanaotumikia vifungo vyao chini ya sheria ya Bodi ya Parole, sura ya 400, sheria ya huduma kwa jamii (sura ya 291) na kanuni za kifungo cha nje.