ANGOLA leo inafanya uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais na wabunge baada Bunge na chama tawala cha MPLA kuridhia masharti ya anayeondoka madarakani, Rais Jose Eduardo Dos Santos.
Kabla ya kukubali kung’atuka, Rais Dos Santos alitoa masharti kwamba ataendelea kuwa Mwenyekiti MPLA hadi mwisho wa maisha yake na asishtakiwe kwa kosa lolote alilofanya akiwa madarakani, kabla ya kuingia madarakani na baada ya kutoka madarakani.
Katika masharti hayo, mrithi wa Dos Santos haruhusiwi kuteua mkuu wa Majeshi, mkuu wa Polisi, mkuu wa Idara ya Ukachero, mkuu wa taasisi ya kupambana na ufisadi, wala mkuu wa magereza.
Wakuu wa taasisi hizo waliopo ambao wameteuliwa na Dos Santos wataendelea kuhudumu kwenye nafasi zao kwa miaka nane zaidi na ikitokea wamefariki ni Dos Santos ndiye atakayeteua wengine.
Masharti mengine ni mali zake na za mtu yeyote kwenye familia yake haziruhusiwi kuhojiwa popote na pia mke wake na watoto wake hawatashtakiwa.
Aidha, famia yake itaendelea kutumia visa za hadhi za kibalozi katika safari za kimataifa na yeye mwenyewe kuendelea kuenziwa kama Rais wa kwanza, baba wa taifa na mkombozi wa taifa hilo.
Dos Santos mwenye umri wa miaka 75 sasa aliingia madarakani mwaka 1979 (akiwa na umri wa miaka 37) na amehudumu kama Rais wa Angola kwa miaka 38 akiwa ndiye Rais aliyekaa muda mrefu zaidi madarakani baada ya Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea.
Binti wa kwanza wa Dos Santos, Isabela Dos Santos ni mwanamke tajiri zaidi Afrika akitajwa na Jarida la Forbes kuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola za kimarekani Bilioni 4.5, sawa na sh trilioni 10 za kitanzania.
Mwanamama huyo ni mkurugenzi mtendaji (CEO) wa Kampuni ya SONANGOL, kampuni iliyopewa kandarasi ya kusimamia uzalishaji wa gesi na mafuta nchini Angola.
Mwaka 2011 kampuni hiyo iliingia kwenye kashfa ya ufisadi wa Dola za Marekani Bilioni 32 (sawa na sh trilioni 70), pesa za mafuta ambazo serikali ililipwa kupitia SANANGOL.
Shirika la fedha duniani (IMF) lilieleza kwamba pesa hizo zililipwa kati ya mwaka 2007 hadi 2010 na kampuni mbalimbali zinayochimba mafuta nchini humo, lakini hazikuingizwa katika vitabu vya hesabu za serikali na hadi sasa hazijulikani zilipo.
Isabela pia anamiki asilimia tano ya hisa kwenye kampuni ya kuzalisha saruji nchini humo ya Nova Cimangola na pia ana hisa asilimia 29 katika Kampuni ya ZON Multimedia.
Ni mjumbe wa bodi wa benki mashuhuri ya BIC, akimiliki asilimia 23 ya hisa za benki hiyo na pia anamiliki asilimia 20 ya hisa katika benki ya taifa ya uwekezaji ya Ureno (Banco Português de Investimento) kupitia kampuni yake ya Santoro Holding.
Aidha, ni mwanahisa katika kampuni zingine ya mafuta nchini humo.
Chama tawala cha MPLA kinapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda kikiwa na viti 175 bungeni huku chama kikuu cha upinzani UNITA kikiwa na viti 32, na vyama vingine vikiwa na jumla ya viti 13.
Jumla ya watu milioni tisa9 wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa leo.
Chanzo mitandao