Bandari ya Dar es Salaam imepanda kwa nafasi 105 katika Ripoti ya Ufanisi wa Bandari Duniani (Container Port Performance Index – CPPI) ya mwaka 2025 na kuwa miongoni mwa bandari zenye ufanisi mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo inayotolewa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na S&P Global Market Intelligence, Bandari ya Dar es Salaam imepanda kutoka nafasi ya 360 mwaka 2024 hadi nafasi ya 255 mwaka 2025 duniani.

Akizungumzia matokeo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za kuboresha huduma za bandari na kupunguza muda wa meli kusubiri na kuhudumiwa.

Amesema ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kwa takribani asilimia 98 kutokana na kupungua kwa muda wa kuhudumia meli, hali inayotarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza kasi ya mizigo kufika sokoni na kuimarisha ushindani wa biashara.

Hata hivyo, amesema pamoja na mafanikio hayo, TPA inaendelea kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za bandari kwa kuwekeza zaidi katika upanuzi wa miundombinu katika bandari zake zote.

Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha bandari za Tanzania zinaendelea kutoa huduma bora na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania pamoja na nchi zinazotumia huduma zake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here