Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel John Nchimbi, amezihimiza wizara za kisekta nchini kujumuisha fursa za biashara ya kaboni katika mipango yao ili kuchangia uhifadhi wa mazingira na kuharakisha maendeleo endelevu.

Akizungumza Juni 5, 2026, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, Dkt. Nchimbi alisema biashara ya kaboni ni nyenzo muhimu inayoweza kusaidia sekta mbalimbali kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi huku ikichochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

Ameeleza kuwa matumizi sahihi ya fursa za biashara ya kaboni yanaweza kuongeza uwezo wa nchi katika kuhifadhi mazingira, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia miradi yenye kuzingatia maendeleo ya kijani.

Makamu wa Rais pia aliwapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa ajenda ya nishati safi nchini, akisema mchango wao umeongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira huku akibainisha kuwa matumizi ya nishati safi yana nafasi kubwa katika kupunguza uharibifu wa mazingira, kuhifadhi misitu na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Nchimbi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi ili kuhakikisha malengo ya uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi yanafikiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani mwaka 2026 yamehitimishwa leo yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, “Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here