Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, ameagiza mashirika ya umma kujitegemea na kuacha kutegemea ruzuku za Serikali, akisisitiza kuwa taasisi hizo zinapaswa kufanya kazi kwa tija, ufanisi na kuleta faida kwa taifa.

Dkt. Mwinyi amesema bado kuna mashirika yanayoendeshwa kwa fedha za Serikali ikiwemo mishahara ya watumishi, hali ambayo amesema imepitwa na wakati na haiendani na kasi ya maendeleo ya uchumi wa kisasa. Amesema Serikali haitakuwa tayari kuendelea kubeba taasisi zinazoshindwa kujiendesha.

Akizungumza leo Mei 23, 2026 wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma lililofanyika katika Golden Tulip Zanzibar Airport, Rais Mwinyi amesema Serikali itatoa muda kwa mashirika hayo kufanya mageuzi ya kiutendaji ili yaweze kujiendesha kwa ufanisi na kuongeza mchango katika maendeleo ya taifa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi na uimarishaji wa bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo na miundombinu ya barabara ili kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uchumi wa kisasa na endelevu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwinyi amesema hana nia ya kuongeza muda wa urais zaidi ya kipindi kilichowekwa kikatiba, huku akiagiza kusitishwa kwa mijadala yote kuhusu suala hilo.

Amesema viongozi wameapa kuilinda Katiba ya nchi na kwamba nguvu kubwa zinapaswa kuelekezwa katika kuwahudumia wananchi na kuharakisha maendeleo badala ya kujadili masuala yasiyo na tija kwa taifa kwa sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here