Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameongoza zoezi la usafi wa mazingira jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani pamoja na mashindano ya Africa Cup of Nations.

Zoezi hilo lililofanyika leo Mei 23, 2026 lilianzia eneo la Uwanja wa Ndege wa Terminal One hadi Chuo cha Utumishi, ambapo viongozi pamoja na wananchi walishiriki kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mazingira ya jiji yanakuwa safi na salama wakati wote ambapi miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kutenga maeneo maalum kwa wafanyabiashara ili kuondoa biashara holela zinazochangia uchafuzi wa mazingira na msongamano wa watu na magari barabarani.

“Tunataka Dar es Salaam ibaki kuwa safi muda wote. Ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kulinda mazingira kwa kuacha kutupa taka ovyo na kufuata utaratibu uliowekwa wa kufanya biashara katika maeneo yaliyotengwa,” amesema Mpogolo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amesema zoezi la usafi linaendelea kila siku kupitia wakandarasi wa usafi wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya jiji huku Halmashauri inaendelea kushughulikia changamoto ya kuziba kwa mitaro pamoja na kuondoa taka zilizokusanywa katika baadhi ya maeneo kufuatia mvua zilizonyesha hivi karibuni.

Aidha, amesema matumizi ya zana za kisasa za usafi wa michanga barabarani yameanza kuleta matokeo chanya katika kuboresha mazingira ya jiji hilo. Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na wakandarasi wa usafi ili kuhakikisha Dar es Salaam inabaki kuwa safi na yenye kuvutia kuelekea AFCON pamoja na shughuli nyingine za kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here