Rais wa Bassirou Diomaye Faye amemfuta kazi Waziri Mkuu Ousmane Sonko kupitia amri ya rais iliyotangazwa Ijumaa kwenye runinga ya taifa, hatua inayomaliza miezi kadhaa ya mvutano wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili.

Hatua hiyo imekuja baada ya Sonko kumkosoa waziwazi Rais Faye katika kikao cha maswali na majibu bungeni, hali iliyoongeza sintofahamu kuhusu mgawanyiko wa madaraka ndani ya serikali ya Senegal. Sonko, ambaye anaungwa mkono kwa nguvu na vijana wengi nchini humo, ndiye aliyemchagua Faye kuwa mgombea wa urais mwaka 2024 baada ya yeye mwenyewe kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo.

Baada ya taarifa ya kufutwa kazi kutolewa, mamia ya wanafunzi wa Cheikh Anta Diop University waliingia mitaani jijini Dakar kuonyesha kumuunga mkono Sonko. Kupitia mtandao wa X, Sonko alisema ana amani baada ya kuondolewa madarakani akisema, “Alhamdulillah. Usiku wa leo nitalala nikiwa na amani katika mtaa wa Keur Gorgui.”

Licha ya kuondolewa serikalini, Sonko bado ana nguvu kubwa kisiasa baada ya chama chake kushinda viti 130 kati ya 165 katika Bunge la Taifa. Wiki hii pia wabunge wa Senegal walipitisha marekebisho ya sheria za uchaguzi yatakayoruhusu watu waliowahi kupatikana na makosa madogo kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, hatua inayotajwa kufungua njia kwa Sonko kushiriki uchaguzi wa urais wa mwaka 2029.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here