Shirika la ndege la Uganda Airlines limetangaza kusitisha kwa muda safari zake za kwenda na kutoka Kinshasa kufuatia hofu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea katika eneo hilo.

Katika taarifa iliyotolewa na usimamizi wa shirika hilo, uamuzi huo umeanza kutekelezwa rasmi kuanzia Mei 23, 2026 hadi itakapotolewa taarifa nyingine. Shirika hilo limesema hatua hiyo imechukuliwa kama tahadhari ya kulinda afya, usalama na ustawi wa abiria, wahudumu wa ndege pamoja na wananchi kwa ujumla.

Uganda Airlines imewataka abiria walioathiriwa na kusitishwa kwa safari hizo kuwasiliana na idara ya huduma kwa wateja ili kupata msaada na maelekezo zaidi kuhusu safari zao.

“Tunasikitika kwa usumbufu wowote utakaojitokeza kutokana na hali hii na tunashukuru kwa uelewa na ushirikiano wa wateja wetu katika kipindi hiki,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, shirika hilo limesema litaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mlipuko huo kwa kushirikiana na mamlaka za afya pamoja na sekta ya usafiri wa anga, huku taarifa zaidi zikitarajiwa kutolewa kadri hali itakavyokuwa ikiendelea.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Uganda kuthibitisha visa viwili vya maambukizi ya Ebola aina ya Bundibugyo vilivyoingia kutoka nje ya nchi na kuhusishwa na mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya Uganda, Diana Atwine, amesema mmoja wa wagonjwa hao amefariki dunia huku mgonjwa mwingine akiendelea kupata nafuu baada ya vipimo vya Mei 18 na Mei 20 kuonyesha hana tena maambukizi ya Ebola.

Kwa mujibu wa Atwine, watu 127 waliokaribiana na wagonjwa hao tayari wametambuliwa na kuwekwa katika karantini maalum ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo nchini Uganda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here