Uganda imethibitisha visa vitatu vipya vya ugonjwa wa Ebola huku mamlaka za afya zikiongeza juhudi za kuwafuatilia watu waliokutana na waathiriwa hao ili kuzuia kuenea kwa maambukizi nchini humo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko wa aina adimu ya virusi vya Ebola Bundibugyo kuwa dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi kimataifa, likionya kuwa hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ipo katika kiwango cha juu sana.
Kwa mujibu wa WHO, takriban visa 750 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola pamoja na vifo 177 vimeripotiwa nchini Congo ambako ndiko kitovu cha mlipuko huo. Shirika hilo limesema changamoto za kuchelewa kugundua wagonjwa, ukosefu wa chanjo au tiba maalum, pamoja na vurugu za kutumia silaha na uhamaji mkubwa wa wananchi vinaongeza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo.
Visa vipya vilivyothibitishwa nchini Uganda vinahusisha dereva aliyemsafirisha mgonjwa wa kwanza wa Ebola pamoja na mhudumu wa afya aliyepata maambukizi wakati akimhudumia mgonjwa huyo.
Wizara ya Afya ya Uganda imesema wagonjwa hao wawili wanapatiwa matibabu huku wakiwa tayari wametambuliwa miongoni mwa watu waliokuwa wamewasiliana na mgonjwa wa kwanza.
Kisa cha tatu kinamhusu mwanamke kutoka Congo aliyewasili Uganda akiwa na dalili ndogo za tumbo kabla ya kusafiri kutoka Arua karibu na mpaka hadi Entebbe, na baadaye kutafuta matibabu katika hospitali binafsi jijini Kampala.







