Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kuboresha usafiri, kuongeza ufanisi wa uchukuzi na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi nchini.
Dkt. Nchemba amesema hayo leo Jumamosi Mei 23, 2026 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Mchepuo ya Mji wa Iringa (Iringa Municipal Bypass) yenye urefu wa kilomita 7.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami katika mkoa wa Iringa.
Baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya barabara nchini kwa lengo la kuimarisha uchumi pamoja na kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi.
Amesema barabara hiyo itasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa msongamano wa magari katika mji wa Iringa, hususan eneo la mlima wa Ipogoro ambalo limekuwa likikumbwa na changamoto za ajali na msongamano kutokana na ongezeko la magari na shughuli za usafiri.
Katika hatua nyingine, Dkt. Nchemba amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Serikali kuhakikisha wanawalipa kwa wakati wakandarasi wadogo, mafundi pamoja na vibarua wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuimarisha ustawi wao na kuongeza ufanisi wa kazi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga barabara za mchepuo katika miji mikubwa ili kupunguza msongamano wa magari na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo nchini.
Awali akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Kaimu Meneja wa tanroads Mkoa wa Iringa, Hosea Machaka amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 38.5 huku kazi mbalimbali zikiendelea ikiwemo ulipuaji wa miamba, ujazaji wa kifusi, ujenzi wa makalavati pamoja na njia za mchepuo.







