Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uboreshaji wa huduma za Bandari ya Dar es Salaam kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari hiyo.
Akizungumza baada ya Kamati hiyo kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa bandarini hapo Mei 23, 2026, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Masanja Kadogosa amesema wajumbe wa Kamati wameridhishwa na maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya bandari, hususan ongezeko la kasi ya huduma za ushughulikiaji wa shehena.
Amesema maboresho hayo yamewezesha kuimarika kwa ufanisi wa bandari hiyo na kuongeza uwezo wake wa kuhudumia mizigo kwa haraka zaidi, hatua inayochochea ukuaji wa biashara na uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa ameishukuru Kamati ya PIC kwa kufanya ziara hiyo na kujionea kazi kubwa inayotekelezwa na Serikali katika kuimarisha sekta ya bandari nchini.
Profesa Mbarawa amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika maboresho ya miundombinu ya bandari, mifumo ya kisasa ya uendeshaji pamoja na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha bandari za Tanzania zinaendelea kuwa kitovu muhimu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.
Aidha, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maoni, ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo yatafanyiwa kazi kwa lengo la kuongeza zaidi ufanisi wa huduma bandarini na kuimarisha mchango wa sekta ya bandari katika kukuza uchumi wa Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Ports Authority, Plasduce Mbossa amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na maboresho ya miundombinu ili kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo mingi zaidi kwa wakati.
Amefafanua kuwa maboresho hayo yamechangia kuongezeka kwa mapato ya ndani ya TPA pamoja na kuimarisha ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia masoko ya nchi jirani zinazotegemea bandari hiyo kama lango kuu la biashara.







