Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amezindua mradi wa basi dogo unaoendeshwa na vijana wa kikundi cha UNAMA katika kijiji cha Picha ya Ndege, wilayani Mkuranga. Mradi huo unalenga kutoa huduma ya usafirishaji na kuongeza ajira kwa vijana.
Mwang’onda aliwapongeza vijana hao kwa kurejesha mkopo wao wa awali, hatua iliyowawezesha kupata nyongeza ya mtaji wa shilingi milioni 85.2 kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri. Alisisitiza kuwa mikopo hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya vijana na taifa.
Naye Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, amesema mikopo hiyo imekuwa fursa ya kweli kwa vijana kujiajiri, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wake kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo Bi.Khadija Nasir amesema Mwenge wa Uhuru 2026 umekagua miradi nane yenye thamani ya shilingi milioni 39.5 wilayani humo, ukiwemo miradi ya nishati safi, maji, elimu na viwanda, na utaendelea na mbio zake wilayani Kibiti.














