Rais Samia amezindua meli hiyo leo Aprili 25,2026 kwenye ufukwe wa Makao Makuu ya Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) Kigamboni mkoani Dar-es-salaam na kusema kuwa hatua hiyo inalenga kukuza fursa za ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha lishe.
“Niipongeze Serikali ya Japan kwa kushirikiana nasi katika kutengeneza meli hii na kupitia wao kwa kushirikiana na UNDP tutapata boti mbili za kasi ambazo zitasimamia doria ya uvuvi wa bahari kuu.” Amesema Rais Samia.
Aidha amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta ya Uvuvi kupitia ujenzi wa bandari za uvuvi ikiwemo ya Kilwa ambayo imefikia asilimia 97 na Bagamayo ambazo zote kwa pamoja zinalenga kuimarisha uchumi, ajira na usalama wa chakula.
Mbali na hayo Rais samia ametoa maelekezo mbalimbali kwa wizara ikiwa ni pamoja na kutunza meli hiyo, kutatua changamoto za wavuvi wadogo zinazohusu mitaji na mazingira ya kufanya shughuli zao, kutoa elimu ya usimamizi wa fedha kwa wavuvi ili fedha wanazopata ziwanufaishe na kutumia sheria na taratibu kwenye usimamizi wa uvuvi endelevu na badala ya nguvu na mabavu.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk. Bashiru Ally amemshukuru Rais Samia kwa jitihada za kuendeleza sekta ya Uvuvi nchini ambapo ameeleza kuwa Meli hiyo ni sehemu ya Meli nyingine 4 zinazotarajiwa kununuliwa na Serikali ili ziimarishe uvuvi wa bahari kuu.






