BEIRUT, Lebanon
SAHAU kwa muda kile kinachoendelea kati ya Marekani na Iran. Kwenye kona nyingine ya Mashariki ya Kati, kuna vita vingine vinavyoendelea kwa ukali mkubwa—vikihusisha Israel na wapiganaji wa Hezbollah wa Lebanon.
Kwa miaka mingi, Hezbollah imekuwa moja ya maadui wakubwa wa Israel. Mwaka 2023, baada ya Hamas kuivamia Israel, Hezbollah waliingia kwenye mzozo huo kwa madai ya kuisaidia Hamas, kundi la Palestina linalopambana na Israel.
Na hali hiyo imejirudia tena mwaka 2026. Tangu Februari 28, 2026, baada ya Israel na Marekani kuanza mashambulizi dhidi ya Iran, Hezbollah wamejitokeza tena na kuanza kushambulia Israel, wakidai kuwa wanatetea mshirika wao wa karibu, Iran.
CHIMBUKO LA HEZBOLLAH
Hezbollah ilizaliwa katika mazingira ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoitikisa Lebanon kwa miaka 15 kuanzia mwaka 1975. Vita hivyo vilitokana na migawanyiko ya kidini na kisiasa iliyokuwa imejengeka kwa muda mrefu.
Mwaka 1943, Lebanon ilifanya makubaliano maalumu ya kugawana madaraka kwa misingi ya dini. Ilikubaliwa kwamba:
• Waislam wa Sunni watatoa Waziri Mkuu,
• Wakristo watatoa Rais,
• Waislam wa Shia watatoa Spika wa Bunge.
Lakini mgawanyo huo haukuleta utulivu wa kudumu. Baadaye mvutano uliongezeka, hasa baada ya wahamiaji kutoka Palestina kuingia nchini humo kwa wingi, hali iliyowaongezea nguvu Waislam wa Sunni. Upande mwingine, jamii ya Shia ilianza kushikamana zaidi na baadhi ya Wakristo wachache ili kujilinda kisiasa na kijamii.
Wakati huo huo, Israel ilianza kuingilia Lebanon kwa madai ya kuwasaka wapiganaji wa Palestina waliokuwa wakijificha Kusini mwa Lebanon na kutumia maeneo hayo kama kambi ya kupanga mashambulizi dhidi ya Israel.
Katika mazingira hayo, Iran iliingia na kuanza kutoa msaada mkubwa kwa Waislam wa Shia, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kijeshi, silaha na fedha, kwa lengo la kupambana na uwepo wa Israel nchini Lebanon.
Ndipo kundi hilo lilipojipanga upya na baadaye likajitambulisha rasmi kwa jina la Hezbollah, maana yake ikiwa ni “Chama cha Mungu” (The Party of God).
Mwaka 1985, Hezbollah waliweka wazi malengo yao makuu:
1. Kuondoa ushawishi wa mataifa ya Magharibi katika ardhi ya Lebanon.
2. Kulisambaratisha Taifa la Israel.
3. Kuifanya Lebanon kuwa Taifa la Kiislam, huku raia wengine wakipewa uhuru wa kuabudu.
Kwa sasa, Hezbollah inaungwa mkono zaidi na Waislam wa Shia, na inaelezwa kudhibiti maeneo muhimu ya Lebanon ikiwamo sehemu kubwa ya Beirut, Kusini mwa Lebanon, na maeneo ya Mashariki mwa Bonde la Bekaa.
MAPAMBANO YA MUDA MREFU NA ISRAEL
Kwa muda mrefu, Hezbollah na Israel wamekuwa kwenye mapigano ya mara kwa mara, hali iliyosababisha majeraha, vifo na uharibifu mkubwa kwa pande zote.
Hata hivyo, mwaka 2025 kulifikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Lakini makubaliano hayo hayakudumu muda mrefu.
Februari 2026, Hezbollah walirejea vitani tena baada ya Israel na Marekani kuanza mashambulizi dhidi ya Iran, wakisema hawawezi kukaa kimya wakati mshirika wao mkubwa akishambuliwa.
UONGOZI NA NGUVU YA KIJESHI
Septemba 2024, Hezbollah walipata pigo kubwa baada ya shambulizi la anga la Israel kumuua kiongozi wao wa muda mrefu, Hassan Nasrallah.
Nasrallah alijulikana kwa misimamo yake mikali na uwezo wake wa kuhamasisha wafuasi. Pia alisifika kwa mchango wake mkubwa katika kampeni ya kuondoa wanajeshi wa Israel Kusini mwa Lebanon.
Lakini msiba haukuishia hapo. Siku chache baadaye, kabla ya msaidizi wake wa muda mrefu Naim Qassem kukabidhiwa rasmi uongozi, kiongozi mwingine wa juu wa Hezbollah, Hashim Safieddine, naye aliuawa mjini Beirut.
Kwa mujibu wa taarifa za kiusalama, Hezbollah inaaminika kuwa na wapiganaji zaidi ya 500,000, pamoja na uwezo mkubwa wa zana za kijeshi, ikiwamo ndege zisizo na rubani na silaha nzito.
Inaelezwa kuwa silaha zao nyingi hutengenezwa au kusaidiwa na mataifa kama China, Urusi, Iran na Syria. Syria pia imewahi kuwatumia wapiganaji wa Hezbollah katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la IS (Islamic State).
NAFASI YA HEZBOLLAH KATIKA SIASA ZA LEBANON
Tofauti na makundi mengi ya wapiganaji duniani, Hezbollah haijabaki porini pekee. Imekuwa sehemu ya mfumo rasmi wa Serikali ya Lebanon.
Kundi hilo liliingia Bungeni rasmi mwaka 1992, baada ya wanachama wake nane kushinda uchaguzi. Tangu mwaka 2005, limekuwa likipata nafasi za uwaziri ndani ya Serikali.
Katika maeneo inayodhibiti, Hezbollah imekuwa ikitoa huduma za kijamii kama:
• ujenzi wa shule,
• hospitali,
• barabara na miundombinu ya usafiri,
• pamoja na misaada ya kijamii kwa wananchi.
Kwa mtazamo huo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaamini huduma hizo zimewapa mvuto mkubwa kwa raia, hasa maeneo yenye umasikini.
Utafiti wa mwaka 2020 uliwahi kuonesha kuwa takribani asilimia 80 ya raia walihojiwa waliridhishwa na uwepo wa Hezbollah.
Hata hivyo, upande mwingine wa raia unaona kundi hilo limekuwa chanzo cha machafuko, na kwamba limekuwa likiiingiza Lebanon kwenye migogoro ya kimataifa isiyoisha.
TASWIRA YAKE KIMATAIFA
Kimataifa, Hezbollah imekuwa ikitazamwa kwa jicho la wasiwasi na mataifa mengi ya Magharibi.
Tangu mwaka 1997, wakati Marekani ikiwa chini ya Rais Bill Clinton, Hezbollah iliwekwa rasmi katika orodha ya makundi ya kigaidi duniani.
Baadaye, katika miaka ya 2010, chini ya Rais Barack Obama, Marekani iliongeza ushirikiano na msaada kwa Jeshi la Lebanon kwa lengo la kudhibiti nguvu ya Hezbollah.
Vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Hezbollah na watu wanaohusishwa nayo viliendelea chini ya utawala wa Joe Biden na sasa vinaendelea pia chini ya Rais Donald Trump.
Kwa upande mwingine, Hezbollah imekosolewa pia na Umoja wa Ulaya (EU), pamoja na baadhi ya wanachama wake wakuu kama Uingereza na Ujerumani, ambao wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali dhidi ya kundi hilo.
HITIMISHO
Kwa kifupi, Hezbollah ni kundi lenye sura mbili:
Kwa baadhi ya raia wa Lebanon, ni “mkombozi” na mlinzi wa jamii ya Shia.
Kwa upande wa mataifa ya Magharibi na Israel, ni kundi la kivita linaloleta hofu na kuendeleza migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati.
Na kadri mvutano kati ya Israel, Marekani na Iran unavyoendelea, ndivyo Hezbollah inavyozidi kubaki kuwa mchezaji mkubwa katika vita vinavyoathiri usalama wa dunia.






