Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo (Mb) amewasili Jijini Istanbul, nchini Uturuki kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 152 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utakaofanyika tarehe 15 hadi 19 Aprili, 2026.
Mhe. Sillo amewasili usiku wa kuamkia leo tarehe 13 Aprili 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Istanbul na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari, Naibu Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Uswisi, Balozi Dkt. Hoyce Temu na Mwakilishi wa Katibu wa Bunge la Tanzania kwenye Mkutano huo, Ndg. Daniel Eliufoo.
Mhe. Naibu Spika anaongoza Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano huo wa siku 5 akimwakilisha Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu.
Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Uturuki, Mhe. Recep Tayyip Erdoğan na unawakutanisha Wabunge kutoka nchi 183 wanachama.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine unatarajiwa kujadili masuala ya mazingira na hali ya ulinzi na usalama duniani na uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo.











