Monday, December 23, 2024
spot_img

KESI YA HEROIN YA MUNA, HARIRI NANI WA KUMFUNGA PAKA KENGELE?

NA CHARLES MULLINDA

BADO sijamuona mtu wa kumfunga paka kengele ili kutanzua mtanziko uliopo sasa katika mjadala mkali unaohusu kushindwa kwa serikali katika kesi ya dawa za kulevya iliyokuwa ikiwakabili wapenzi wawili, Mohamed Hariri na Muna Said.

Ninachokiona ni hofu, wasiwasi, woga, vitisho na upigaji ramli. Niliowaalika kujibu maswali mepesi yanayoulizwa sasa na wachokonozi huku uswahilini hawajajitokeza hata mmoja. Wote wamenyaza.

Walisoma maandishi ya mchokonozi na kuyaelewa vema maswali mepesi aliyowauliza makachero wa kesi ya unga ya Muna na Hariri kisha wakanyamaza. Wakanyamaza kimya kabisa. Kimya cha msibani.

Waliojitokeza ni wapiga porojo. Baadhi wameeleza mshangao wao kwa kusoma maandishi ya kichokonozi yakiwa na maswali mepesi ambayo eti! Hayajibiki!

Eti, kwao wao maandishi hayo ya kichokonozi hayakupaswa kuandikwa katika jukwaa hili na kusomwa na maelfu ya watu kwa sababu kufanya hivyo ni kuwaanika wahusika.

Wengine wamejitokeza wakichekea kwapani huku wakigongeana viganja vya mikono yao kwa furaha ya kusoma andiko linalofikirisha. Eti! wanaulizana mchokonozi ni nan!? Watu wa ajabu sana.

Wapo walioogopa na kunivaa wazima wazima kwa sauti zilizojaa hofu zilizokuwa zikinong’ona kuwa ninachokoza nyuki; na wachache wamethubutu kuninyooshea kidole cha ole. Eti! Nisithubutu tena. Wanaponda kokoto kwenye chuma cha pua.

Ndiyo kwanza nimeanza kuandika, maandishi yangu ni mepesi na yanayofurahisha kuyasoma! Sina mamlaka ya kuhukumu wala sijahukumu yeyote.

Nilichofanya ni kuchangia mjadala uliohudhunisha wengi ambao msingi wake ni fedheha iliyoipata serikali kwa kushindwa mahakamani katika Kesi ya unga. Sasa weweseko ni la nini?

Muna na Hariri sasa ni raia huru baada ya kuibwaga serikali mahakamani lakini wachokonozi hawazuiliwi kusemezana kuhusu mwenendo wa kesi yao.

Kesi nzito nzito na za kukata na shoka kama hii ya Muna na Hariri na kwa upande mwingine serikali, mwenendo na hukumu zake hutumiwa kufundisha vyuoni na pia hutumiwa na majaji na mahakimu kama rejea wanapohukumu watu wema na waovu.

Ndivyo ilivyo hata kwa wachokonozi, Kesi hii ni darasa la kukata na shoka ambalo mwanafunzi akilielewa vizuri anaweza kujinasua katika vitanzi vigumu.

Tutakuwa tunatenda dhambi ambayo haiwezi kutolewa hukumu mahakamani kama tutaanza kutapatapa kuhusu hatma ya Muna na Hariri kwa sababu tu ya mjadala unaohusu ushindi wao dhidi ya serikali.

Wanaoweweseka sasa baada ya mjadala huu kupewa hadhi ya kichokonozi ya kuwa kesi darasa wanatulazimisha wachokonozi tujiulize kuwa, kama hakukuwa na tatizo katika mwenendo mzima wa kesi hadi hukumu, kwanini wameanza kutapatapa na kujiuliza ni wapi kinakotokea kiherehere cha mchokonozi kuipa hadhi kesi hii iliyomalizika kwa kutoa ushindi kwa washitakiwa?


Itoshe tu kueleza msimamo wangu hapa kuwa nitaendelea kuandika kuhusu kesi hii kwa sababu sasa ninaamini zipo kesi nyingi za aina hii au zinazokuja ambazo pengine, serikali itashindwa mahakamani.

Nitaendelea kuandika ili kuitoa serikali tongotongo za macho, iweze kuona kama zipo kesi nyingine ambazo haiwezi kushinda zifutwe kuliko kuendelea nazo na mwisho kushindwa kwa  fedheha.

Kwa wachokonozi wenzangu, naweka agano nanyi kuwa sitakiuka makubalino yetu kwa kuendelea kuhoji maswali mepesi kabla sijapata majibu ya maswali mepesi niliyouliza siku chache zilizopita.

Sitauliza kama kile kinachozungumzwa sasa huko uswahili kuwa eti! Muna ndiye alikuwa kiungo mchezeshaji katika kesi hii na sitathubutu kuhoji popote kuwa tangu kukamatwa kwa kiungo huyo mchezeshaji, Muna, na kukaa msambweni zaidi ya mwaka mmoja alikuwa akitembelewa kila mara na kina nani?

Mchokonozi ni mtu wa agano. Nimeweka agano nanyi. Ninawaachia makachero wajiulize wenyewe na waje na majibu ni nani hasa aliyekuwa akifika gerezani mara kwa mara kumtembelea Muna? Mtu huyo alikuwa ndugu yake? rafiki yake? binamu yake wa hiari, shemeji yake au msamalia mwema?

Siyo kazi yangu kuwafundisha makachero kazi ya ukachero hivyo ninawaachia wenyewe kutafuta tarehe, mwezi na mwaka ambao Muna aliingia gerezani.

Mfanyabiashara Mohamedi Hariri, ambaye ameibwaga serikali mahakamani katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya kukamatwa na unga pamoja na mkewe Muna Said


Wanajua makachero na naamini watajua kama hizi tetesi za huku uswahili kwa wachokonozi kuwa kipindi chote cha Corona ambapo hakukuwa na ruhusa ya wageni kwenda magereza kusalimia, ni akina nani walikuwa wakikiuka utaratibu huo?

Haya ni maandishi ya mkono wangu mchokonozi ambayo hayataruka karatasi hii kwa sasa kwenda ya pili kuhoji ni akina nani kule gerezani waliokuwa wakitoa ruhusa kwa wageni kuingia gerezani wakati kulikuwa na zuio?

Tukutane wiki ijayo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya