MCHOKONOZI
MOYO wangu umekaa upogo, fikra zangu zimeganda, mwili wangu umelegea, usingizi wangu umekuwa wa shida. Ninahisi kuitapika roho yangu.
Mimi ni mpenzi wa kahawa iliyotiwa sukari ya kutosha, mchana na usiku kinywaji changu ni hicho. Mapenzi haya yamegeuka mateso, mchana ninateswa na sukari ninapoiunga kwenye kahawa ya Africafe, usiku ninateswa na jinamizi la tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kuhusu kiungo hiki; Sukari.
Wala mimi simtuhumu mtu, bali ninateseka mwenyewe na kisa cha mateso haya ni sukari na tuhuma za Mpina. Sukari kila ninapoiona mchana ninakasirika, ninatamani kuimwaga, moyo wangu unasawajika. Ninapolala usiku ninaota ndoto. Ninaota ninakabwa na jinamizi la tuhuma zilizomwangwa mchana kweupe na Mpina. Tuhuma nzito kweli kweli.
Kahawa
Nimejaribu bila mafanikio kuichukia sukari kwa sababu ni tamu na nimeshindwa kabisa kumchukia Mpina kwa sababu kila ninakopita huku uchokonozi, jina lake linaimbwa kwa mapambio ya sifa za uzalendo na ushujaa, Mpina amekuwa mzito. Mpina ametikisa. Wasifiaji wa Mpina wanasifu kutoka moyoni, hawaimbi sifa za kinafiki.
Nimeshindwa kuwa na akili za kiuendawazimu za kupuuza hoja kadhaa katika tuhuma zilizoibuliwa na Mpina kwenye skandali ya sukari. Sitaki kuwa punguani kiasi cha kushindwa kujiuliza karatasi, simu, kompyuta na sukari wapi na wapi?
Katika mateso yangu haya nimegundua miaka mingi ijayo historia itamtaja Mpina kama mbunge shujaa wa nyakati za sasa. Mpina ameandika jina lake katika vitabu vya historia. Wachokonozi ametuachia maswali yasiyokuwa na majibu. Hatujui nani wa kuyajibu kwa sababu hajatokea wa kuyajibu huku uchokonozi. Maswali ya Mpina yanatutesa.
Ninapolala, haraka usingizi unanichukua na hapo naoto ndoto, naota nakabwa na jinamizi la tuhuma zilizotolewa na Mpina kuhusu skandali ya sukari. Ninaota vijana wa kizazi cha kuhoji, miaka mingi ijayo watakapokuwa wakisoma vitabu vya historia na kukutana na skandali hii ya karne ya sasa watavyolazimika kutafuta majibu ya maswali yanayoulizwa sana hivi sasa huku uchokonozini.
Ninawaona katika ndoto vijana wakisoma sheria ya sukari, sura ya 251 ya mwaka 2020 inayosema Bodi ya Sukari haitaruhusiwa kutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi hadi ijiridhishe kwamba uzalishaji wa ndani upo chini ya kiwango kinachohitajika na kwamba kazi hiyo itafanywa na wazalishaji wa ndani wenye sifa zinazotakiwa.
Wakiwa wamekodoa macho, wanasoma baadhi ya sifa hizo kuwa ni kusajiliwa na bodi, kuwasilisha mpango wake wa mwaka wa uzalishaji wa sukari na kuutekeleza kwa angalau asilimia 80 katika mwaka uliopita wa msimu wa uzalishaji.
Wanasoma pia kuwa mzalishaji sharti awe na uwezo wa kuzalisha si chini ya tani elfu kumi kwa mwaka na kuwa na rekodi nzuri ya kutimiza masharti ya uagizaji sukari kutoka nje.
Historia itasomeka kuwa taarifa iliyotolewa na Mpina kwa wachokonozi enzi hizo kulikuwa na uhaba wa tani 30,000 za sukari kama ilivyoandikwa kwa maandishi na bwana sukari lakini wao wakasema uhaba wa sukari ulikuwa tani 60,000. Nikiwatizama vijana hawa wanaposoma ni kama wanasema potelea pote labda wao hao hawakulala vizuri siku hiyo kwa sababu siku hazilingani.
Lakini vijana wanaposoma kuwa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kwa wanaoruhusiwa kisheria vilitolewa Mei 3, 2023 na kuisha Juni 30 mwaka huo huo hivyo waagizaji hao walishindwa kuagiza sukari kwa sababu ya muda mfupi uliotolewa; naziona sura zao zikianza kubadilika kwa mshangao. Wanawashanga waliotoa kibali cha kuagiza sukari ndani ya muda huo mfupi kuwa nia yao hasa ilikuwa nini?
Usingizi ni mzito, naota vijana wanasoma nondo za Mpina zinazoeleza kuwa baada ya kutokea uhaba wa sukari, Kampuni ya Zenj General Merchandise Company bila kufanyiwa uhakiki kuhusu uwezo wake na uhalali wake wa kufanya kazi na serikali iliruhusiwa kuingiza nchini tani 60,000 za sukari na mara moja wanapayuka; hii ni skandali.
Luhaga Mpina
Nikiwa naota nawaona vijana wakipekua kurasa kwa kurasa kutafuta majibu au sababu za uamuzi huu lakini hawayapati. Tuhuma hizo nzito zinabaki kuwa tuhuma ambazo majibu yake hayapo. Wanafyonya kwa hasira. Wanaendelea kusoma.
Sasa wanasoma nukuu inayosema wao hao walitoa kibali kwa kampuni iliyosajiliwa na wakala wa Usajili Biashara na Mali Zanzibar Januari 5, 2016 kabla ya kusajaliwa BRELA kisha Januari 5, 2024 ilifungua Ofisi Mtaa wa Nyasubi, Kahama Shinyanga halafu April 2, 2024 ikapewa kibali cha kuingiza nchini tani 10,000 za sukari. Naota nikisema haya ni maajabu ya Musa maana hata neno linalopendwa kutumiwa na Andrew Chenge halitoshelezi kubeba uzito wa maajabu haya.
Nimelala fofofo, naota vijana wanasoma nondo za Mpina kuwa Kampuni ya J Square Investiment Group Company ambayo usajili wake ni kuuza vifaa vya shuleni na ofisini, huduma za upishi wa vyakula na usafi wa mazingira kuwa nayo ilipewa kibali cha kuingiza tani 2,500 za sukari.
Haraka wanarejea kwenye sheria ya sukari, sura ya 251 ya mwaka 2020 inayosema Bodi ya Sukari haitaruhusiwa kutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi hadi ijiridhishe kwamba uzalishaji wa ndani upo chini ya kiwango kinachohitajika na kwamba kazi hiyo itafanywa na wazalishaji wa ndani wenye sifa zinazotakiwa. Hawaendelei kusoma zaidi sheria hiyo, nawaona nyuso zao zinasawajika na mimi naiona roho yangu inarukaruka kama inataka kuuacha mwili.
Malaika
Wanapenda kusoma. Wanaendelea kusoma palipoandikwa kampuni ya kuuza simu kwa rejareja, kompyuta, TEHAMA na vifaa vingine vya mawasiliano inayoitwa ITEL East Africa Limited nayo ilipewa kibali cha kuagiza tani 60,000 za sukari huku kukiwa hakuna mahali panapoonyesha kuwa ilipata kuomba kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi. Wanauma midomo. Kila neno la honyo linawatoka mdomoni, adabu inawaponyoka. Hawasomi tena.
Naota wasomi hawa wakitoka mbio kukimbilia vichakani kuchuma fimbo, wanarudi mbio na fimbo zao mikononi na kuanza kuyacharaza makaburi ya waliolala ili kupoza hasira zao za kukosa majibu ya sababu za uamuzi huo. Wanaliita jina la Mungu wao wakimsihi ajitokeze ili wafungue mashtaka kwake kumuomba aunde Tume Tukufu ya Malaika kuja kusaka majibu ya maswali haya.
Kabla sijaamka naota maswali yanayoulizwa sasa na wachokonozi lakini hayajajibiwa, kwamba kwanini sukari iliagizwa zaidi ya mara nne ya mahitaji halisi na kwanini tani 410,000 za sukari ziingizwe nchini bila kulipiwa kodi ya ongezeko la thamani VAT wakati sukari ya ndani inatozwa kodi?
Uchokonozini wanauliza wazalishaji wa ndani watashindana vipi kwenye soko ambalo kuna sukari ya nje inayouzwa bila kulipiwa kodi? Na kwamba eti kwani wao hao hawaoni kuwa sukari kutoka nje ya nchi inaua viwanda vya ndani na kudumaza ustawi wa kiuchumi wa wakulima na wafanyakazi?
Boksi
Hapo jinamizi la tuhuma za Mpina linanikaba kwa nguvu mpaka naanza kuhisi kuishiwa pumzi, mateso haya ya ndotoni yanakuwa makali. Nikiweweseka; nikiwa katika weweseko hilo, nawaona wachokonozi maelfu kwa maelfu wamembeba juu Mpina wakikimbia naye kwenda kwenye boksi.
Kufika hapo, mahali paliposafishwa pakawa safi, peupe pee; hakuna wadudu wachafu watambaao wala warukao, wachokonozi wanamsimamisha Mpina pembeni ya boksi hilo, wanaanza kutumbukiza karatasi nyeupe zilizoandikwa kwa wino wa kijana jina la Luhaga Joelson Mpina, huku wakiimba – jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni.