Monday, December 23, 2024
spot_img

WAZIRI NAPE LIA NAO, CHEKA NAO, WAKIFA WAOMBOLEZEE

MCHOKONOZI

CHARLES MULLINDA

NAPE Moses Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninakuandikia waraka huu wa Mchokonozi ili mioyo ya waandishi wa habari itakapokuwa inalia, urejea kuusoma ulie pamoja nao, watakapokuwa wakikenua meno yao kwa furaha nawe uliachie tabasamu lako mwanana uchekelee pamoja nao.

Waziri Nape, waandishi wa habari wanaokufia na watakaondelea kukufia mikononi mwako uwaombolezee kwa moyo wa baba anavyomuomboleza mwanaye mpendwa kwa namna ambayo umekuwa ukifanya tangu MAMA alipokuketisha kwenye kiti hicho; na kwa wale watakaobahatika kufika mbele ya Mwenyezi Mungu, atakapokuwa akiwakaribisha katika ufalme wake, walitaje jina lako kwa ukamilifu na kwa herufi kubwa, NAPE MOSES NNAUYE ili Mungu Mwenyezi alisikie kwa usahihi.

Nape, naomba uniruhusu nikuite kwa jina ulipopewa na wazazi wako la Nape kwa sababu ndiyo utamaduni wa Mchokonozi kuamini katika undugu badala ya kusujudiana, kusifiana na kukwezana kusikokuwa na maana sana. Jina ulilopewa na wazazi wako lina heshima duniani na mbinguni na ndilo lililo kwenye daftari la Mwenyezi Mungu. Haya majina mengine ya nyongeza ni ya shuleni, vyuoni, ofisini, bungeni na kwenye maeneo yanayofanana na hayo. Mungu hayatambua majina hayo.

Ninakuandikia mawazo yangu Mchokonozi ili kukufikirisha, mimi na wewe tufikiri pamoja, wewe na wanahabari wote unaowalea na kuwaongoza mfikiri pamoja. Siandiki hapa kukupinga, kukukosoa wala kukufundisha. Mimi Mchokonozi ni nani hata nithubutu kutenda hayo? Sina udhu huo.

Nape, Mintarafu na nyadhifa ulizopata kuwa nazo katika Taifa letu, wewe unaijua vema Safu ya Mchokonozi. Haujakutana nayo barabarani, umeishi nayo ukiiongoza kwa miaka ya kutosha na kwa sababu Mwenyezi Mungu ilimpendeza kukuumba na karama ya uongozi, mapenzi yake yatimizwe.

Nape, ninakuandikia waraka huu ili tufikiri pamoja kuhusu mwenendo wa Sekta ya Habari hapa nchini wakati huu ukiwa umeunda kamati ya watu tisa uliyoipa jukumu la kufanya tathimini ya hali ya uchumi katika vyombo vya habari na ukiwa umewezesha sheria mpya ya habari kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni. Ninasisitiza ninaandika ili tufikiri pamoja na si vinginevyo.

Nape ninataka mimi, wewe na waandishi wote tuutizame msalaba uliopewa na MAMA wa kuongoza tasnia hii kwa namna ulivyo mzito pengine kuliko misalaba yote uliyopata kukutana nayo katika maisha yako ukizingatia nia yako njema ya kutaka kujenga umoja na upendo kwa wanahabari jambo ambalo sidhani kama utafanikiwa; kuwapigania wawe na maisha bora vita ambayo sidhani kama utaishinda; kunusuru anguko la kiuchumi la vyombo vya habari jambo ambalo ni gumu sana na mema mengine yote uliyoyakusudia kuyafanya ukiwa umeketi kitini hapo.

Nape, ukweli unauma lakini ukweli ni dawa na tena ukweli huponya, usikilize; Ninaandika kukuuma sikio kuwa kama zilivyo tasnia nyingine, tasnia ya habari unayoingoza nayo ina watu masikini kupitiliza, wema, wanafiki, wanaopendana, wasiopendana, wanaoaminika na wasioaminika na labda ndiyo tasnia inayojiangamiza yenyewe.

Tambua kuwa tasnia ya habari inayotambulika kuwa mhimili wa nne wa Dola imegawanyika katika makundi ya vyama vya siasa. Hivi sasa kuna magrupu ya wana habari ya mitandaoni kulingana na ushabiki wa vyama vya siasa, yapo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yapo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ya Chama cha ACT Wazalendo na mengineyo.

Viongozi wa magrupu hayo wanaitwa maadimini na kazi yao kuu ni kusambaza propaganda za vyama wanavyoshabakia. Akitokea mwandishi akaweka kwenye grupu taarifa ya chama ambacho admini si chawa wake au hata inayokosa au kutofautiana na chama au kiongozi wa chama anachoshabikia, admini atamsakama na hata kumfukuza kundini.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye

Inasemekana maadimini hawa wanaishi kwa kazi hiyo ya uadimini kwa sababu uandishi wa habari haulipi. Eti! Wanayatumia magrupu hayo kujiingizia kipato, kuchafua waandishi wenzao wanaotofautina nao kimsimamo na mitizamo na wapo waliojiongeza wakawakusanya viongozi mbalimbali wakawaweka kwenye grupu moja la mtandaoni kisha wakajipa uadimini. Hawa ukikosana nao watakuchafua na kukupaka masizi kwa hao wakubwa. Uadimini unawalipa, wana viriba tumbo.  

Waandishi wako hapo ndipo tulipofikia, tumekuwa waandishi wa vyama vya siasa na wanasiasa, waandishi wa mabwanyenye, waandishi wanaowindana na kuchafuana kwa sababu ya njaa, waandishi wabeba mikoba ya wakubwa, taaluma tuimetupa kando. Watanzania wanatuona kwa sababu haya hayafanyikii gizani, wanaidharau taaluma na wana taaluma. Tumeinajisi tasnia. Ni nani anapenda najisi? Ndiyo maana tupo kama unavyotuona.

Nape, baadhi ya vyombo vya habari vilivyopo sasa vinafanya kazi ya ukuwadi na kujikomba. Vinajikomba kwa MAMA na Serikali yake, vinashindana kumsifia MAMA, kuwasifia ninyi mawaziri na wakubwa wengine. Vyombo vya habari vinavyotimiza wajibu wake sawasawa wa kuelimisha, kukosoa, kukemea nk, kama vipo ni jambo la kumshukuru Mungu. Navyo havipo salama sana kwa sababu chawa wapo kazini.

Kusifia si jambo baya lakini kusifu kuliko pitiliza ni kuchafua. Ni zaidi ya uchawa. Wasomaji na wasikilizaji wa vyombo vyetu vya habari vipo wanavyovidharau kwa sababu wameviweka kwenye kundi la chawa. Binadamu au chombo cha habari na chawa wapi na wapi? kwa sababu tumejipa sifa ya uchawa, tumeachwa tuwe chawa.

Wewe ni mwanataaluma Nape, kiongozi na mjuvi hasa wa mambo ya habari. Najua unalijua hili kuwa wasomaji na wasikilizaji wakishakidharau chombo cha habari kwa sababu ya kujivika uchawa kinakosa wateja, kikikosa wateja kinayumba kiuchumi, lakini mbaya zaidi hata yule anayesifiwa naye akishajua kuwa chombo cha habari kile ni chawa wake naye anakidharau, anajua hakina lolote la maana zaidi ya kumsifia. Kwani ni nani anayempenda chawa ingawa ni rahisi kutaja jina lake?

Nape siku hizi kuna waandishi wa habari na maafisa habari. Kuna vita ya maafisa habari na waandishi wa habari. Kimsingi, hawa wote ni waandishi wa habari lakini kwa hali ilivyo sasa waandishi wa habari halisi ni walioko kwenye vyumba vya habari na wale waliosomea uandishi wa habari kisha wakaajiriwa serikalini au kwenye taasisi, mashirika na kampuni ambako wana uhakika wa kupata mlo wao wa kila siku, hao ni maafisa habari.

Leo, katika mjadala huu tuwaweke kiporo waandishi wa habari, tuanze na maafisa habari, twende pamoja: Moja ya majukumu ya msingi ya maafisa habari ni kuwa daraja la upatikanaji habari baina ya wanahabari na taasisi wanazozifanyia kazi na; maafisa hawa ndiyo wenye mamlaka ya kutoa au kushawishi kwa wakubwa wa taasisi wanazozitumikia kutoa matangazo kwa vyombo vya habari.

Nape, baadhi ya maafisa habari hawa sasa ni miungu watu kwa waandishi wa habari na nadhani wanachangia kwa kiasi kikubwa anguko la kiuchumi la wanahabari na vyombo vya habari na hata upatikanaji wa habari za ofisi walikoajiriwa.

Wapo ambao hawajiamini, wapo wenye roho mbaya kwa sababu walizaliwa nazo, wapo wajasiriamali wanaozitumia ofisi waliko kuvuna nje ya mishahara yao na lakini; wapo maafisa habari ambao ni waandishi wa habari. Hawa ndiyo wale walionyooka kama uzi kwenye kazi zao. Ni watu clean, kwao nyeupe ni nyeupe na kekundu ni kekundu, wanajiamini kwa waandishi wenzao na kwa wanaofanya nao kazi huko waliko. Hawa hawana mbwembwe na wala hawajitakatifuzi, ni waandishi wa habari haswa.

Maafisa habari wasiojiamini wana wasiwasi wakati wote, hata kutoa kauli nyepesi kabisa au kujibu maswali rahisi ya wanahabari wanaoomba taarifa kwao ni lazima iwe vita. Hawa huweka ukuta wa chuma unaozuia kuwafikia mabosi wao na ikitokea habari ikaandikwa bila kauli ya upande wa pili ambao ni wao, wanakuwa wa kwanza kulalama kuhusu maadili ya uandishi wa habari kutozingatiwa.

Waandishi wa habari wakiwa kazini

Haya yanapotokea mabosi na wafanyakazi wa kada nyingine katika taasisi waliko hubaki wakishangaa na wengine wakiwacheka waandishi wa habari kwa jinsi wanavyoumizana wenyewe kwa wenyewe. Huwa wanawadharau waandishi wa habari.

Maafisa habari wenye roho mbaya wao hawataki mafanikio ya wandishi wa habari wengine au chombo cha habari, wanataka wao tu ndiyo wawe na maisha bora huku waandishi wenzao wakiendelea kusaga soli kwenye barabara za lami.

Hawa ndiyo wale ambao kila barua za kuomba matangazo au matoleo maalumu kutoka vyombo vya habari zinazofika mezani kwao huwa wanazitupa kapuni. Yaani wao hawataki mwingine apate; nao ndivyo walivyo. Hawa nao ni kundi muhimu sana linaloshiriki bila ā€˜soniā€™ kudumaza na kuua kabisa uchumi wa vyombo vya habari na wanahabari wenyewe.

Lakini kuna hili kundi lingine la maafisa habari wajasiriamali. Hawa ni wale ambao kazi zote za kihabari ambazo zina mwanya wa kumnufaisha mwandishi wa habari au chombo cha habari huwa wanazifanya wao bila kujali kama wana uwezo huo au hawana.

Safari zenye posho kwa waandishi wa habari wanaziziba; angalia ziara wanazoziandaa na kuita wahariri kama kweli huleta tija inayopaswa; fanya tathimini ndogo ya posho zinazolipwa na habari au makala zinazoandikwa kwenda kuuelimisha au kuupasha habari umma kama vinaendana. Matangazo, eti! nao hupenda walau wapate asilimia 10 au 15. Chochote kile kinachohusisha kumnufaisha mwanahabari au chombo cha habari hukiziba. Wanafaidi huku wakiwaangamiza kiuchumi waandishi wenzao na kuua vyombo vya habari.

Mbali na hao, wapo maafisa habari ambao ni waandishi wa habari. Hawa ndiyo wenye mafanikio makubwa kwenye ofisi zao, huwezi kusikia migogoro baina yao na waandishi wenzao na hata kwenye ofisi walizoko wanaheshimika na maafisa wenzao na mabosi wao. Ni chanzo cha habari cha uhakika cha vyombo vya habari. Hawa wanafahamika. Hakuna sababu ya kuwasifia sana wasije wakaanza kuharibu huko tuendako.

Nape, nisikuchoshe. Kabla sijaweka kalamu yangu chini kwa leo turejee alichokisema Mhariri Absalom Kibanda siku ya Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022, lililofanyika Disemba mwaka jana jijini Dar es Salaam; Tuanze. ā€˜Mwaka 2016/2017 kidogo nilipata tofauti na Rais wetu wa zamani, Dk. John Magufuli nilipojaribu kumshauri kwamba ni vizuri turithi kile ambacho marais wastaafu walitufundisha sisi katika Sekta ya Habari.

ā€˜Wanahabari tumepata kutoa Rais ambaye ni mwandishi wa habari ambaye ni Benjamin Mkapa, alikuwa very critical kwa media lakini alitoa fursa sana kwa media kupata taarifa.

ā€œTunaongea kuhusu fake news leo katika mitandao, thanks God Dk. Rioba na ndugu yangu Mike wamefanya rejea na kututhibitishia kuwa fake news hazijaanza na mitandao ya kijamii au online media, ni historically toka media imeanza na fake news kwa hiyo misinformation na disinformation zipo pale.

Absalom Kibanda

ā€˜Lakini njia kubwa na muhimu au tuseme nini kifanyike. Kwanini wakati wa Mkapa kwa mfano, wakati wa Rais Kikwete kulikuwa na kiwango kidogo cha fake news hata katika main stream media. Kwa sababu kulikuwa na diversity.

ā€˜Leo hii, inatokea fake news, vyombo vya habari havipo na havipo kwa maana kweli kweli. Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan yuko Marekani, ameandamana na waandishi wangapi? nani wa Daily News yuko na Rais? nani wa TBC yuko na Rais? nani wa Mwananchi yuko na Rais? nani na Azam yuko Rais? nani wa Clouds yuko na Rais?

ā€˜Hicho ndiyo chanzo cha fake news, misinformation na disinformation. Rais wetu alikwenda ku rauch royal tour, kwa mambo ya ajabu kabisa, unamuona Msemaji Mkuu wa Serikali akihojiwa na … yaani Gerson Msigwa anamuhoji Dk. Abbas. What kind of journalism is that, we are killingā€¦. Kwa sababu tunafungua wigo au pandorral box ya fake news, misinformation na disinformation kwa sababu hatutumii vyombo vyetu vya habari vilivyopo, waandishi wetu wa habari waliopo kwa manufaa yale.

ā€˜Unaweza kujiuliza leo, je hakuna akina Reginald Mengi tena? akina Mbunguni wengine? akina Joseph Kusaga wengine? Kwanini media zote ambazo zinaanzishwa leo ni media za entertainment na sports? Kwa sababu upande huu wa Serious News tumeua.

ā€˜Leo hii kuna waandishi wakongwe hapa, nilihudhuria press conferes ya Rais George Bush Marekani mwaka 2003, wakati huo nilikuwa na miaka 40 kidogo huko, mimi ndiyo, i was the youngest journalist pale, waandishi ambao ni correspondent wa state house kutoka media mbalimbali, CNN, ni zaidi ya miaka 60 lakini wana waandishi vijana wadogo wako.

ā€˜Leo hii vyombo ya habari Tanzania, kuna generation gap, kuna vijana wadogo, hawa akina Halima Sharifu hawapo. Nani anawalea kitaaluma ndani ya vyombo vya habari, lakini kwanini media inashindwa, kwa sababu Serikali ambaye ndiye mdau mkuu imeacha kujihusisha na media.

ā€˜Leo hatuna uwezo. Kama katika royal tour, Rais aliweza ku raise seven billion, je watu wa habari katika Serikali walishindwa kutenga milioni 200 kupeleka waandishi wa habari kuandamana na Rais kule Marekani? kuandamana na Rais Arusha, Dar es Saalam na Zanzibar kwenye rauch?

Yaani mna own mnasema maelezo TV ndiyo inafanya covarage na sio Mwananchi au Azam, nafikiri hapo ndipo tulipokosea. Nadhani nimetoa dokezo tu.ā€™

Mchokonozi

Nape, mimi na wewe tulikuwepo kwenye kongamano hilo, maneno haya ya Kibanda tuliyasikia. Na haya ndiyo yatatuongoza kwenye mjadala wetu huu wiki ijayo. Tukutane jumapili ijayo

ITAENDELEA.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya