RIPOTA PANORAMA
MRADI wa kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme wa kilovoti 400 vya Chalinze, Pwani na Zuzu – Dodoma umezinduliwa.
Mradi huo utakapokamilika utasambaza umeme unaozalishwa kutoka bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere, kwa lugha ya kimombo Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP) kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Kati na Magharibi, migodini, viwandani na kuimarisha biashara ya umeme katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Akizindua mradi huo juzi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko alisema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia hivi karibuni, Tanzania sasa ni kinara kwa nchi za Afrika katika usambazaji umeme kwa wananchi wake.
Alisema gharama za mradi huo zinatolewa na Serikali kwa asilimia 100 ambayo imekusudia Taifa kuwa na umeme wa uhakika; lengo likiwa kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Dk. Biteko alisema Serikali imeendelee kuimarisha upatikanaji Nishati ya Umeme katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyopo hadi kufikia Megawati 3,169.26 lakini mahitaji ya juu ya umeme nchini kwa sasa ni Megawati 1,888.72.
“Kuimarika kwa uzalishaji wa umeme nchini kumechangiwa na kuanza uzalishaji kwenye mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 99.6.
“Megawati 1,175 za umeme sasa zinazalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa,” alisema Dk. Biteko.
Aidha, Dk. Biteko alitumia fursa hiyo kuwaonya wahujumu wa miundombinu ya umeme kwani wanarudisha nyuma uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.
Aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua kali wahujumu wa miundombinu ya umeme.
Dk. Biteko aliwataka wakandarasi wa mradi huo ambao ni Kampuni ya TBEA ya China kuukamilisha kwa wakati ili wananchi wapate manufaa yaliyokusudiwa.
Wakati huo huo, Dk. Biteko ameukumbusha umma wa watanzania kutumia nishati
safi ya kupikia ili kutimiza lengo la Serikali la asilimia 80 ya
watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Alisema Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu bei ya soko na inasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara.
Dk. Biteko alitoa rai kwa wafanyabiashara kusaidia upatikanaji wa majiko ya gesi na ya umeme kwa bei nafuu na kuyasambaza hadi vijijini.
