RIPOTA PANORAMA
Arusha
ASASI za kiraia (AZAKI) zaidi ya 400 kutoka ndani na nje ya nchi, kesho zinaanza mkutano wao wa kila mwaka jijini hapa huku ajenda ya ushiriki wa vijana katika michakato ya kidemokrasia ukiwa mojawapo ya ajenda kuu za mkutano huo.
Vijana kutoka maeneo mbalilmbali nchini watashiriki katika mijadala itakayowasilishwa katika mkutano huo, utakaohudhuriwa na washiriki 600 kutoka asasi hizo, serikali na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo, Nesia Mahenge amesema kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo huku Naibu Balozi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) nchini, Balozi wa Canada na Meya wa Jiji la Arusha, wakitarajiwa kushiriki katika mkutano huo wa siku tano.
“Pamoja na mijadala kuhusu masuala mbalilmbali yanayogusa jamii, pia tutatembelea shughuli za kijamii katika jamii za pembezoni hasa wanawake wa kimasai,” anasisitiza Nesia ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya CBM International nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa HAKI ELIMU, Dk. John Kalaghe, anasema kuwa vijana watakaoshiriki katika mkutano huo, watazungumza na kujadili umuhimu wa vijana katika michakato ya kidemokrasia nchini, tunapoelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji na uchaguzi mkuu ujao.
“Tunataka vijana watambue umuhimu si wa kushiriki tu michakato ya kidemokrasia bali pia wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalilmbali, wapige kura na hata wasimamie michakato hiyo hasa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani,” anasema Dk. Kalaghe katika mkutano na waandishi wa habari.
Dk. Kalaghe pia amesisitiza umuhimu wa vijana na makundi yote katika jamii kushirikishwa katika kutengeneza dira ya maendeleo ya taifa ya 2050 na kwamba ni muhimu wakaeleza ni mambo gani wangependa yaongezwe na kuboreshwa katika masuala ya kidemokrasia nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi anasema mkutano huo wa mwaka huu utatoa fursa kwa wanawake kutathmini na kutoa sauti zao katika maandalizi ya dira ya taifa 2050
Anasema mkutano huo utatumika kuhamasisha vuguvugu la vijana, hasa wanawake waliopo mashule kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.
“Utafiti unaonyesha kuwa viongozi wanawake ni asilinia mbili kwa maeneo ya vijijini na asilinia sita mijini, idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya wanawake nchini hivyo uhamasishaji unahitajika sana,” amesema.
Anasema kuwa katika mkutano huo kutakuwa na kigoda cha mwanamke mmasai ambacho kitawasaidia wanawake wa pembezoni kupaza sauti zao na kushiriki katika dira ya taifa 2050.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Bora Initiatives, Ishmail Biro anasema kuwa umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa na dira ya taifa 2050 ni kutokana na wingi wao,kwa mujibu wa sensa ya idadi ya watu ya mwaka2022.
“Asilinia 75 ya idadi ya watu nchini ni vijana wenye umri chini ya miaka 35 hivyo wanastahili kuhamasishwa washiriki kugombea, kupiga kura na kusimamia uchaguzi katika ngazi zote za kisiasa.
“Dira ya Taifa ya 2050 inawahusu zaidi vijana kuliko makundi mengine katika jamii hivyo ushiriki wao ni muhimu na thamani ya michango yao inambulika ,” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Foundation for Civil Society (FCS), Justin Rutenge amesema kwamba Dira ya Taifa 2050 inapaswa kushirikisha kikamilifu makundi yote katika jamii wakiwamo vijana,wanawake na hata watoto.
“Dira ya Taifa ya 2025 iliiandaliwa zaidi na wataalamu lakini hii ya 2050 inapaswa kushirikisha na kuzingatia maoni ya makundi yote katika jamii,”anasema.
Mkuu wa idadi ya sekta ya umma katika Benki ya Stanbic, Doreen Dominic ametaka Taasisi nyingine binafsi kuunga mkono hatua ya benki hiyo ya kudhamini mikutano ya namna hiyo kutokana na umuhimu wake kwa taifa.
Kauli mbiu ya mkutano mkuu wa mwaka huo wa Asasi hizo ni Sauti,Dira na Thamani.






